Iran yaonya juu ya kuendelea kuuziwa silaha Saudia, Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i17437-iran_yaonya_juu_ya_kuendelea_kuuziwa_silaha_saudia_israel
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu kuendelea kuuziwa silaha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa hatua hiyo itakuwa na maafa makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 15, 2016 08:13 UTC
  • Iran yaonya juu ya kuendelea kuuziwa silaha Saudia, Israel

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu kuendelea kuuziwa silaha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa hatua hiyo itakuwa na maafa makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akihutubu katika mkutano wa kila mwaka wa Kamati ya Kimataifa ya Usalama ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Gholam-Hossein Dehqani, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika umoja huo amesema kuendelea kuziuzia silaha Saudia na Israel kutachangia kuendelea ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhujumiwa mipaka ya nchi zingine za eneo hili la Mashariki ya Kati.

Mashambulizi ya anga ya Saudia nchini Yemen

Dehqani amebainisha kuwa, utawala wa Aal-Saud unatumia mabomu, makombora na silaha nyinginezo kutoka Marekani na Uingereza, katika hujuma zake za kinyama dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen, ambapo watu zaidi ya 10,000 wameuwa hadi sasa. Kadhalika amesema kuna udharura wa kuushinikiza utawala haramu wa Israel kujiunga na mkataba wa NPT unaozuia utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa silaha za atomiki akisisitiza kuwa, silaha za nyuklia zinazomilikiwa na utawala huo wa Kizayuni ndio silaha hatari zaidi katika eneo hili.

Silaha za nyuklia za Israel

Uchunguzi wa taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI), ambao ripoti yake ilitolewa Februari mwaka huu ulionesha kuwa, kiwango cha usafirishaji nje silaha kimeongezeka kwa asilimia 14 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku Marekani ikiongoza kwa kusafirisha nje silaha.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Saudi Arabia inashika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Mashariki ya Kati.