Rouhani: EU yawania kurejesha uhusiano na Iran baada ya JCPOA
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Umoja wa Ulaya zipo mbioni kurejesha na kuimarisha uhusiano wao na Tehran, tokea yafikiwe mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Akiwahutubia waandishi wa habari mjini Tehran akiwa pamoja na Rais wa Finland Sauli Niinistö, Rais Rouhani amesema nchi za Ulaya zimeongeza kasi ya kuimarisha uhusiano na Iran katika nyuga za uchumi, sayansi na teknolojia, haswa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. Mapatano hayo ya nyuklia yalitiwa saini Julai 2015 baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani Julai 14 mwaka jana 2015.
Kwa upande wake, Rais Sauli Niinistö wa Finland amesema anaamini sasa uhusiano wa Tehran na Helsinki utaimarika maradufu baada ya taifa hili kuondolewa vikwazo huku akiyataja makubaliano hayo ya nyuklia kama 'hatua nyeti.'
Amesema Iran na Finland zipo katika nafasi nzuri ya kuimarisha ushirikiano wao katika nyuga za nishati na teknolojia ya habari na mawasiliano akisitiza kuwa nchi mbili hizi zimekuwa na uhusiano mzuri wa kihistoria, haswa kwa kuzingatia kuwa Iran ilikuwa moja ya nchi za kwanza kutambua uhuru wa Finland.
Mbali na masuala hayo ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, marais wa Iran na Finland wamezungumzia matukio ya hivi sasa haswa katika eneo la Mashariki ya Kati. Wawili hao wamesema kuna haja ya kuwepo ushirikiano wa kimataifa katika kulikabili jinamizi la ugaidi katika nchi za Iraq, Syria, Libya na Yemen.