"Jinai za Marekani ziwekwe paruwanja kimataifa"
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ameitaja Marekani kama adui nambari moja wa Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza udharura wa kuanikwa hadharani jinai za Washington kimataifa.
Akizungumza kwenye hotuba za Sala ya Ijumaa hii leo mjini Tehran, Ayatullah Mohammad Ali Movahedi Kermani amesema iwapo dunia itajua na kufahamu uadui na jinai za kutisha za Marekani, basi nchi za eneo hili la Mashariki ya Kati zitagundua hadaa ya nchi hiyo ya kibeberu na zitambue kwamba ni muhali kunufaika na uhusiano wa pande mbili na Washington.
Ayatullah Kermani amesema walimwengu hawajapata kufahamu rangi halisi ya Marekani haswa namna inavyokiuka mikataba na makubaliano ya kimataifa.
Akiashiria makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1, Khatibu wa Sala ya Ijumaa hii leo mjini Tehran amebainisha kuwa, makubaliano hayo yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) hayajakuwa na maana na manufaa kwa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba hilo limezidi kuipa nguvu hoja kuwa Marekani katu haiheshimu makubaliano yoyote na wajibu wake wa kimataifa.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi Kermani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafaa kutafuta suluhu ya ndani kwa changamoto zake badala ya kuitegemea Marekani.
Kauli ya Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran imetolewa siku chache baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuashiria uadui wa Marekani katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa kukumbuka kutekwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran uliojulikana kama "Pango la Ujasusi".
Akihutubia hadhara ya wanafunzi na wanachuo siku ya Jumatano, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa uadui na ukiukaji wa ahadi wa serikali ya Washington sio jambo geni kwa taifa la Iran na kusisitiza kuwa, utambulisho wa mfumo wa Marekani mkabala na Iran haujabadilika licha ya kupita miaka 38 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kuwa, sera na dhati ya Marekani imejengeka juu ya msingi wa ubeberu na kwa miaka mingi dola hilo la kibeberu limetekeleza siasa zake hizo katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan magharibi mwa Asia na Iran.