Rais Rouhani asisitiza umoja kwa ajili ya kupambana na ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuimarishwa umoja na mshikamano kwa ajili ya kuimarisha usalama na amani ya Mashariki ya Kati.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo wakati wa kufungua Maonyesho ya Kimataifa ya 22 ya Magazeti mjini Tehran. Amegusia hali ngumu inayotawala eneo la Mashariki ya Kati kwa sasa na kusema kuwa, usalama wa eneo hilo hauwezi kuimarishwa bila ya kuwepo mshikamano na umoja katika kupambana na magaidi na maadui.
Rais Rouhani amesema kuwa, matatizo ya sasa ya usalama ni ugaidi na fikra za kijahilia zinazopewa sura na rangi ya mafundisho ya dini na kwamba makundi yenye ufahamu usio sahihi na potofu kuhusu Uislamu yamekuwa yakiua Waislamu kwa kutumia fikra hizo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema vyombo vya habari ni wenzo wa maendeleo ya jamii na kusisitiza kuwa, utamaduni ni wenzo wenye nguvu kubwa kuliko silaha na kwamba vyombo vya habari ndio wenzo wa kiutamaduni.