Marekani yaendeleza siasa za uhasama dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i18886
Tangu mwaka 1979 wakati zilipofichuliwa nyaraka za harakati za siri za ujasusi wa Marekani nchini Iran katika uliokuwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran, rais wa nchi hiyo alitangaza hali ya hatari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2025-07-12T14:05:52+00:00 )
Nov 06, 2016 02:46 UTC
  • Marekani yaendeleza siasa za uhasama dhidi ya Iran

Tangu mwaka 1979 wakati zilipofichuliwa nyaraka za harakati za siri za ujasusi wa Marekani nchini Iran katika uliokuwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran, rais wa nchi hiyo alitangaza hali ya hatari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Sheria inayohusiana na hali ya hatari ilipasishwa na Kongresi ya Marekani na kutiwa saini na rais wa nchi hiyo mwaka 1977. Sheria hiyo inampa rais wa nchi mamlaka ya kutangaza hali ya hatari ya kifaifa kwa ajili ya kukabiliana na hatari kutoka nje dhidi ya usalama wa taifa na kupanga uhusiano wa Marekani kwa mujibu wa hali hiyo. Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali ya Marekani chini sheria hiyo ni pamoja na kusitisha ushirikiano na upande huo, kushikilia mali zake na hata kuzitaifisha kabisa iwapo ardhi ya Marekani itashambuliwa. Hali hiyo ya hatari humalizika yenyewe baada ya kupita mwaka mmoja tangu itangazwe isipokuwa kama rais wa nchi ataiwasilisha tena bungeni siku 90 kabla ya kumalizika kwake.

Rais wa Marekani, Barack Obama

Kwa msingi huo Rais Barack Obama tarehe 3 Novemba iliyosadifiana na tarehe ya kutekwa Pango la Ujasusi la Marekani mjini Tehran (ubalozi wa Marekani), alimwandikia barua Spika wa Bunge la nchi hiyo, Paul Ryan akitangaza kurefushwa tena sheria hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika barua hiyo Obama ametetea hatua yake akidai: "Uhusiano wetu na Iran haujarejea katika hali ya kawaida na utekelezaji wa makubaliano yetu na nchi hiyo haujatimia. Hivyo ninaona kwamba, kuna udharura wa kurefushwa sheria hii kuhusiana na Iran".

Baada ya makubaliano ya Iran na 5+1, 2015

Baada ya kufeli mradi bandia kuhusu madai yaliyohusiana na faili la nyuklia la Iran na kutiwa saini makubaliano ya JCPOA kati ya Jamhuri ya Kiislamu na kundi la 5+1, Marekani ilionesha kwamba, haiko tayari kuachana na sera zake za kihasama na kiadui dhidi ya taifa la Iran. Suala hilo lilionesha tena kwamba, mwenendo wa Marekani bado haujabadilika na kwamba kilichobadilika ni mbinu na utekelezaji wa uhasama na uadui wa nchi hiyo. 

Kurefushwa kwa sheria ya hali ya hatari ya Marekani dhidi ya Iran kumefanyika kwa malengo mawili. Kwanza ni kudumisha mradi wa propaganda chafu na sera za kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio. Hii ni licha ya kwamba, iwapo tutatupia jicho utendaji wa Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha nusu karne iliyopita tutaona kuwa, ni siasa na mienendo ya Washington ambayo daima imekuwa tishio kwa usalama na amani ya Iran. Marekani imekuwa ikitishia usalama wa Iran na usalama wa eneo zima la Mashariki ya Kati kupitia njia ya kutuma majeshi na kuzivamia nchi jirani kama Iraq na Afganistan na athari mbaya za mashambulizi na uvamizi huo ni kupanuka ugaidi katika eneo hilo. Katika kipindi chote cha miongo mitatu iliyopita, Marekani imezitumbukiza nchi za Mashariki ya Kati, kaskazini mwa Afrika na Asia ya kati katika vita na migogoro ya kikabila na kimadhehebu na daima imekuwa ikizuia kuwepo maelewano, umoja na mapatano baina ya Iran na baadhi ya nchi za eneo hilo kwa shabaha ya kuuza silaha za mabilioni ya dola kwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.

Sera za Marekani za propaganda chafu dhidi ya Iran

Lengo la pili la hatua ya Barack Obama ya kurefusha hali ya hatari kuhusiana na Iran ni upinzani laini wa Washington dhidi ya Iran kutazamwa kama nchi yenye nafasi na mchango mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati na katika upeo wa kimataifa. Kwa sasa na baada ya kutiwa saini makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1, Iran imeonekana kuwa na nafasi muhimu zaidi katika masuala ya Mashariki ya Kati, suala ambalo limezidisha uhasama wa Marekani ambao unadhihirishwa katika sura ya kuzusha madai ya urongo kuhusu masuala mbalimbali kama kile kinachoitwa hatari ya makombora ya Iran na madai kuwa Tehran inaunga mkono ugaidi. 

Vijana wenye hasira wa Iran wakichoma moto bendera ya Marekani

Ukweli ni kuwa, dhambi ya Iran kwa Marekani ni uanamapinduzi wa taifa la Iran, misimamo yake huru na ya kujitegemea na kupinga ubeberu na sera za kimabavu za serikali ya Washington na mabeberu wenzake. Ni Wazi kuwa maadamu hali hiyo ingalipo, Iran- katika mtazamo wa Marekani-  itaendelea kutambuliwa kuwa ni tishio kubwa, na kwa msingi huo tutaendelea kushuhudia hatua za kurefushwa hali ya hatari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.