Iran yalaani mashambulizi ya kigaidi Samarra na Tikrit Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i18946-iran_yalaani_mashambulizi_ya_kigaidi_samarra_na_tikrit_iraq
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyopelekea watu wasiopungua 21 kuuawa katika miji ya Samarra na Tikrit nchini Iraq jana Jumapili.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 07, 2016 00:47 UTC
  • Iran yalaani mashambulizi ya kigaidi Samarra na Tikrit Iraq

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyopelekea watu wasiopungua 21 kuuawa katika miji ya Samarra na Tikrit nchini Iraq jana Jumapili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi mbali na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za watu walipoteza maisha katika mashambulizi hayo amesema, jamii ya kimataifa ina jukumu la kukabiliana na ugaidi ulio dhidi ya ubinadamu wa makundi ya wakufurishaji.

Aidha amesema  wafanya ziara kadhaa Wairani wameuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi ya Jumapili asubuhi mjini Samarra na kuongeza kuwa, jinai hiyo inatokana na  magaidi kushindwa katika medani za vita nchini Iraq.

Hujuma ya kigaidi Samarra, Iraq

Qassemi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwa pamoja na serikali na watu wa Iraq hadi watakapopata ushindi kamili katika vita dhidi ya ugaidi.

Duru za habari zinadokeza kuwa wafanya ziara 10 Wairani wamepoteza maisha katika hujuma ya kigaidi mjini Samarra wakati basi lao liliporipukiwa na bomu lililotegwa magaidi.