Nov 27, 2016 07:39 UTC
  • Iran yakosoa utendaji wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na vitendo vya kigaidi

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amekikosoa kimya cha Umoja wa Mataifa kuhusiana na vitendo vya kigaidi na kulitaka Baraza la Usalama la umoja huo kutekeleza majukumu yake ipasavyo kuhusiana na suala zima la ugaidi.

Ghulam Hussein Dehqani amesema hayo katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kiduru wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo sambamba na kuashiria shambulio la kigaidi la siku ya Alkhamisi dhidi ya wafanyaziara katika mji wa Hillah nchini Iraq ametangaza kuwa, shambulio la kigaidi la Daesh si jinai ya kwanza ya kundi hilo la kigaidi dhidi ya Mazuwwar wa Kiirani kwani mara kadhaa wafanyaziara hao wameandamwa na mashambulio ya magaidi hao.

Eneo lilipotokea shambulio dhidi ya Maziwwar Hilla Iraq Novemba 24, 2016

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria jitihada na hatua za Iran katika kukabiliana na magaidi katika Mashariki ya Kati wakiwemo wa kundi la Daesh na kusema kuwa, mashambulio ya kigaidi na jinai kama hizo zimekuwa zikipoteza roho za maelfu ya watu wasio na hatia nchini Syria, Iraq na katika maeneo mengine duniani, suala ambalo linalazimu jamii ya kimataifa kuchukua hatua za maana na athirifu za kuwasambaratisha magaidi.

Ghulam Hussein Dehqani ameukosoa Umoja wa Mataifa kutokana na kunyamazia jinai za kundi la kigaidi la Daesh katika Mashariki ya Kati na kubainisha kwamba, kuenea jinai za matakfiri hao ni kengele ya hatari yenye ujumbe wa udharura wa kuchukuliwa hatua za kuhitimishwa himaya ya baadhi ya nchi kwa kundi hilo la kigaidi na kujiunga katika safu ya kupambana na ugaidi.

Tags