Zarif: Fidel Castro alisimama imara kukabiliana na ubeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20359-zarif_fidel_castro_alisimama_imara_kukabiliana_na_ubeberu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif amesema kuwa, hayati Fidel Castro kiongozi wa zamani wa Cuba aliyefariki dunia alikuwa akisisitiza kuimarishwa ushirikiano na mataifa mengine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 28, 2016 15:12 UTC
  • Zarif: Fidel Castro alisimama imara kukabiliana na ubeberu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif amesema kuwa, hayati Fidel Castro kiongozi wa zamani wa Cuba aliyefariki dunia alikuwa akisisitiza kuimarishwa ushirikiano na mataifa mengine.

Zarif ameyasema hayo leo mjini Tehran kwa mnasaba wa kumkumbuka mwanamapinduzi huyo wa Cuba mbele ya waandishi wa habari. Ameashiria ziara yake ya mwisho mjini Havana alipopata kukutana na Fidel Castro mwenyewe na kusema kuwa kiongozi huyo alieleza wasiwasi wake kuhusu Cuba na nchi nyingine za ulimwengu wa tatu.

Waziri Zarif akiwa na balozi wa Cuba mjini Tehran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Castro alisisitizia uhusiano wa nchi zinazostawi kwa ajili ya kupambana na ubeberu na kuongezwa zaidi juhudi za kujikomboa kutoka kwenye udhibiti wa mataifa yanayopenda kujitanua. Zarif ameongeza kuwa, kifo cha Fidel Castro ni janga kwa harakati za kupigania uhuru hususan katika eneo la Amerika ya Latini na ameeleza matarajio kuona msiba huo unawaunganisha zaidi raia wa Cuba.

Fidel Castro akiwa kijana wakati wa mapambano

Waziri wa mambo ya Nje wa Iran amegusia uhusiano ya karibu sana uliopo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cuba na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizi zinaendeleza uhusiano wao katika nyuga  mbalimbali kieneo na kimataifa.

Kwa upande wake Vladimir Andres Gonzalez Quesada, balozi wa Cuba mjini Tehran akiongea amesema kuwa, Havana na Tehran zina irada kubwa kwa ajili ya kupanua zaidi uhusiano wao.

Fidel Castro, mwishoni mwa uhai wake

Fidel Alejandro Castro Ruz, rais wa zamani wa Cuba alifariki dunia juzi akiwa na umri wa miaka 90.