'Kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji mapatano ya nyuklia'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20611-'kurefushwa_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_iran_ni_ukiukaji_mapatano_ya_nyuklia'
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema muswada wa Bunge la Marekani kurefusha muda wa vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi ni kinyume cha ahadi za Marekani katika mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 02, 2016 12:23 UTC
  • 'Kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji mapatano ya nyuklia'

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema muswada wa Bunge la Marekani kurefusha muda wa vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi ni kinyume cha ahadi za Marekani katika mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa tamko leo Ijumaa kufuatia hatua ya Baraza la Senate la Marekani kurefesha vikwazo vya upande vya nchi hiyo dhidi ya Iran, na kuongeza kuwa, hatua ya kurefushwa vikwazo hivyo ni kinyume cha sheria za kimataifa kuhusu kutoingilia mambo ya ndani na ya kimataifa ya nchi zingine.

Qassemi ameongeza kuwa, serikali ya Marekani inawajibika kutekeleza ahadi zake za kimataifa na matukio ya ndani ya nchi hiyo hayawezi kuwa kisingizio cha kukwepa Washington kutekeleza majukumu yake ya kimataifa.

Aidha amesema Iran inafungamana na mapatano ya kimataifa iliyoyatia saini na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kwa lolote lile. Amesema Iran imejitayarisha kulinda kwa nguvu na kwa hekima haki za Wairani katika hali yoyote ile.

Bunge la Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Tehran inafuatilia kwa karibu hatua zinazochukiliwa na Marekani na kwamba ripoti kamili itawasilishwa kwa jopo la kuratibu mapatano ya nyuklia ili hatua zinazofaa zichukuliwe.

Muswada wa kurefusha muda wa vikwazo dhidi ya Iran kwa miaka kumi zaidi umepasishwa kwa kura 99 za ndio bila ya kuweko kura yoyote ya kupinga katika Baraza la Senate la Marekani jana Alkhamisi.

Tayari Baraza la Wawakilishi limeshapasisha muswada huo ambao sasa unasubiri saini ya Rais wa Marekani kuidhinishwa.

Januari mwaka huu, Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumaini, zilianza kutekeleza makubaliano hayo ya nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 14 Julai, 2015 mjini Vienna nchini Austria.