Dakta Zarif: Usitishaji vita nchini Syria ni mafanikio makubwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i22381-dakta_zarif_usitishaji_vita_nchini_syria_ni_mafanikio_makubwa
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria na kusema kuwa, hatua hiyo ni mafanikio makubwa na muhimu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2016 00:14 UTC
  • Dakta Zarif: Usitishaji vita nchini Syria ni mafanikio makubwa

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria na kusema kuwa, hatua hiyo ni mafanikio makubwa na muhimu.

Dakta Muhammad Javad Zarif amesema katika ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria ni mafanikio makubwa ambapo inawezekana kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kung'oa mizizi ya ugaidi na hivyo kuelekea katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Komandi kuu ya vikosi vya ulinzi vya Syria jana ilitangaza habari ya kufikiwa mapatano ya kusimamisha vita na kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano kote nchini Syria. Ilielezwa katika tangazo hilo kwamba, kuanzia saa sita usiku wa kuamkia leo harakati zote za kijeshi zitasimamishwa nchini humo na kwamba makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhat al-Nusra na yale yenye mfungamano na makundi hayo mawili hayajajumuishwa katika makubaliano hayo.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia alitangaza jana kuwa, mitazamo ya pamoja ya Iran, Russia na Uturuki ndio sababu ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria na kwamba, nchi tatu kwa pamoja zimetoa dhamana ya kutekelezwa makubaliano hayo. 

Wapinzani na serikali ya Syria wamefikia muafaka wa kusimamisha mapigano nchini humo ikiwa zimepita siku kadhaa tu baada ya kukombolewa mji wa kistratejia wa Halab baada ya kudhibitiwa na magaidi kwa zaidi ya miaka minne na miezi mitano.