Rouhani: Makubaliano ya nyuklia ya Iran ni kwa maslahi ya pande zote
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na kundi la 5+1 ni kwa maslahi na manufaa ya pande zote zilizosaini mapatano hayo huko Vienna Julai mwaka 2015.
Akiongea hapa Tehran leo Jumanne, Rais Rouhani amesema makubaliano hayo yaliyopewa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) ni ushindi kwa pande zote husika na kwa maslahi ya eneo zima la Mashariki ya Kati.
Akiashiria matamshi yaliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump kwamba JCPOA ndiyo makubaliano mabaya zaidi katika historia ya sasa duniani, Dakta Rouhani amesisitiza kuwa: "Sisi kama taifa tulifanikiwa kuyashawishi madola makubwa ya dunia kwa kutumia busara, mantiki na heshima hadi yakaridhia kwamba makubaiano haya yana umuhimu na kutekelezwa kwake ni kwa faida ya kila upande na sio tu Iran."
Rais wa Iran Hassan Rouhani amebainisha kuwa, makubaliano hayo ya Vienna yanafaa kutumiwa kama kigezo katika kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu; akitoa mfano hai wa mazungumzo yanayoendelea hivi sasa huko Astana nchini Kazakhstan kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria.
Trump aliwahi kusema wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais kuwa, mapatano ya nyuklia ya Iran ni 'maafa na ni mapatano mabaya zaidi duniani' na kuahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza atakapoingia kwenye Ikulu ya White House.
Mwezi uliopita, Trump alisema makubaliano ya nyuklia ya Iran ambayo yalianza kutekelezwa Januari mwaka jana 2016, hayajakuwa na faida kwa biashara za Marekani na kusisitiza kuwa kuna udharura wa kuvunjiliwa mbali.