Rouhani: Uwezo wa kijeshi wa Iran ni kwa ajili ya kujihami
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema uwezo mkubwa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ni kwa ajili ya kujihami na kulilinda taifa hili kutokana na chockochoko za maadui.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mkutano na mabalozi na wanadiplomasia wa nchi mbali mbali hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa Maadhimisho ya Miaka 38 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi wala haina mpango wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kwamba kujiimarisha kwake kijeshi ni kwa ajili ya kujilinda.
Amesisitiza kuwa, uingiliaji wa kijeshi katika masuala ya ndani ya nchi nyingine ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla.
Dakta Rouhani amefafanua kuwa, adui hawezi kutekeleza vitisho vyake dhidi ya Iran kutokana na uwezo mkubwa wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu.
Kadhalika Rais Hassan Rouhani wa Iran ameongeza kuwa, Tehran inafadhilisha na kutoa kipaumbele kwa uwepo wa uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na mataifa mengine, kwa shabaha ya kufikiwa maslahi ya pamoja.
Tehran imekuwa ikikariri mara kwa mara kuwa, kuimarisha mfumo wake wa makombora ni haki ya taifa la Iran isiyopingika kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa na kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuboresha uwezo wake wa kijeshi kwa lengo la kupambana na wavamizi na maadui.