Rais Rouhani: EU itumie benki za Ulaya kufanya kazi na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25009-rais_rouhani_eu_itumie_benki_za_ulaya_kufanya_kazi_na_iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran na Umoja wa Ulaya zinapaswa kushirikiana na wakati huo huo ametoa mwito kwa benki za Ulaya kuwa na uhusiano zaidi na Iran ili pande mbili ziweze kunufaika na maslahi ya pamoja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 11, 2017 16:42 UTC
  • Rais Rouhani: EU itumie benki za Ulaya kufanya kazi na Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran na Umoja wa Ulaya zinapaswa kushirikiana na wakati huo huo ametoa mwito kwa benki za Ulaya kuwa na uhusiano zaidi na Iran ili pande mbili ziweze kunufaika na maslahi ya pamoja.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumamosi ya leo hapa mjini Tehran katika kikao na waandishi habari akiwa ameandamana na Waziri Mkuu wa Sweden Kjell Stefan Löfven aliyeko safarini hapa nchini. Rais Rouhani ameongeza kuwa: "Baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama "Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), hivi sasa kuna mazingira mazuri ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi baina ya Iran na Umoja wa Ulaya ikiwemo Sweden."

Rais wa Iran amesema katika mazungumzo yake na Stefan wamejadili masuala ya uhusiano wa pande mbili, kitaifa na kimataifa hasa kadhia za Afghanistan, Iraq, Syria na Yemen.

Kwa upande wake Kjell Stefan Löfven  Waziri Mkuu wa Sweden ameashiria ujumbe wa ngazi za juu wa kibiashara alioandamana nao akiwa Tehran na kusema, jambo hilo linaonyesha azma ya nchi yake kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika safari ya  Stefan hapa Tehran, Iran na Sweden zimetiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika sekta kadhaa.