Zimbabwe: Tutaendelea kushirikiana na Iran kutetea Wapalestina
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amezikosoa baadhi ya nchi zinazojiita za Kiislamu kwa kushindwa kusimama kidete kutetea maslahi ya Wapalestina.
Katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Zimbabwe Francis Mudenda hapa mjini Tehran, Dakta Ali Larijani amesema "Ni jambo la kusikitisha namna baadhi ya nchi za Kiislamu licha ya utajiri mkubwa na ushawishi wao katika medani ya siasa za eneo na kimataifa, lakini zimepuuza kabisa kadhia ya Palestina na kufumbia macho dhulma wanazofanyiwa Wapalestina kila uchao na utawala pandikizi wa Israel."
Kadhalika Spika wa Bunge la Iran amempongeza mwenzake wa Zimbabwe kwa kutoa hotuba ya kishujaa na ya kutia moyo, alipozungumza hapo jana katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Zimbabwe ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kubeba benderea ya watetezi wa Palestina sambamba na kuwa mstari wa mbele kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazolikabili eneo hili.
Kadhalika katika mkutano wake na Dakta Larijani, Francis Mudenda amekariri kuwa serikali ya Harare itaendelea kuunga mkono na kutetea Intifadha ya Wapalestina hadi pale mapambano hayo yatakapozaa matunda na Palestina kutangazwa kuwa taifa huru kikamilifu.
Spika wa Bunge la Zimbabwe aidha ameyataka mabunge ya nchi zilizoshiriki mkutano wa kimataifa wa Palestina hapa Tehran yafanye juu chini kuhakikisha kuwa maazimio yote ya kongamano hilo yanatakelezwa, ili kukomesha ukaliwaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina na utawala ghasibu wa Israel kwa takriban miongo 7 sasa.
Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina ulimalizika jana Jumatano hapa Tehran, kwa kuzishirikisha nchi zaidi ya 80 na washiriki zaidi ya 700 kutoka kona zote za dunia.