Mar 01, 2017 07:18 UTC
  • Iran yataka suala la haki za binadamu lisitumiwe kisiasa

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya sheria na ya kimataifa alisema jana kwenye kikao cha Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi kwamba, ni jambo la dharura kwa suala la haki za binadamu kuepushwa kikamilifu na masuala ya kisiasa.

Araqchi amezikosoa hatua za baadhi ya nchi za kutumia suala la haki za binadamu kama wenzo wa kuzishinikiza nchi nyingine kupitia Umoja wa Mataifa na kusema, Baraza la Haki za Binadamu linapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kusimamia haki za binadamu duniani kupitia mazungumzo ya maana na sio kugeuzwa kuwa chombo cha kuzusha mizozo na kutoa tuhuma dhidi ya mataifa mengine.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya sheria na ya kimataifa amegusia pia historia ndefu ya kiustaarabu, kiutamaduni na Kiislamu ya Iran na kusema, Tehran daima imekuwa ikiliweka suala la kuunga mkono na kustawisha haki za binadamu; katika ajenda yake kuu na imechukua hatua nyingi za kivitendo za kufanikisha jambo hilo.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Amesema, Iran siku zote imekuwa ikitoa ushirikiano mzuri kwa Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala la haki za binadamu, hivyo kupasishwa azimio la haki za binadamu kuhusu haki za binadamu nchini Iran katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo ni hatua isiyo na maana na isiyokubalika.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia namna haki za binadamu zinavyovunjwa kupindukia huko nchini Yemen na kusema, jamii ya kimataifa haipaswi kufumbia macho watu wanafanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo sambamba na kuvunja misikiti, shule, mahospitali na nyumba za raia.

Amezungumzia pia jinai zinazofanywa na Israel huko Palestina na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka za kukomesha uvunjaji mkubwa huo wa haki za binadamu.

Tags