Mar 12, 2017 07:27 UTC
  • Iran, Hizbullah zalaani hujuma ya kigaidi mjini Damascus

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika jana Jumamosi katika mji wa Damascus nchini Syria, ambapo makumi ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyataja mashambulizi hayo ya kigaidi kuwa ni kitendo cha kikatili na cha fedheha.

Amesema ugaidi kipofu na mauaji ya halaiki ya watu wakiwemo wanawake na watoto ni ishara ya kutapatapa magenge ya kigaidi baada ya kupata pigo baada jingine na kupoteza ngome zao. 

Wakati huo huo, harakati ya Hizbullah ya Lebanon pia imelaani hujuma hiyo na kusema kuwa, wakati umefika kwa Waislamu, pasina kujali madhehebu zao, waungane dhidi ya magenge ya kigaidi.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Taarifa ya Hizbullah imefafanua kuwa, licha ya magaidi kudai kuwa wanapigana na kufanya harakati zao kwa jina la dini, lakini mara kwa mara wamekuwa wakiwalenga waumini wa Kiislamu wakiwa katika marasimu na shughuli mbalimbali ya kidini. 

Hapo jana mabomu mawili yalilipuka katika mji mkuu wa Syria, Damascus katika eneo la Bab Masala ambapo watu wasiopungua 46, wakiwemo Wairaqi 40 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Hujuma hizo za kigaidi zilifanyika karibu na makaburi ya Bab al Saghir karibu na moja ya milango saba ya Mji wa Kale wa Damascus. Hata hivyo shirika la Syrian Observatory for Human Rights linasema waliouawa katika hujuma hiyo ni watu 59 wakiwemo wafanyaziara 46 aghalabu yao wakiwa raia wa Iraq. 

Magaidi waliwalenga wafanyaziara waliokuwa wanatembelea Haram ya Hadhrat Sukaina SA, binti wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).

Tags