Apr 04, 2017 16:16 UTC
  • Rais Rouhani: Kutokomeza ugaidi kunahitaji juhudi za jamii ya kimataifa

Rais Hassan Rouhani amelaani shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu uliotokea kwenye treni ya chini ya ardhi katika mji wa St. Petersburg nchini Russia na kusisitiza kuwa kuutokomeza ugaidi kunahitaji juhudi za jamii ya kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika ujumbe wa salamu za rambirambi kwa Rais Vladimir Putin wa Russia ambapo mbali na kutoa mkono wa pole kwa serikali na familia za watu waliouliwa na kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi ameeleza kuwa: Kutokomeza ugaidi wa aina zote bila kujali sababu yake kunahitaji jitihada za pamoja za jamii ya kimataifa na ushirikiano wa nchi zote kwa ajili ya kukabiliana na chimbuko la kifikra na waungaji mkono wa makundi hayo watenda jinai.

Dakta Rouhani ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatangaza tena utayari wake wa kushirikiana kwa kila namna na serikali ya Russia katika kupambana na ugaidi.

Eneo la tukio kwenye treni ya chini ya ardhi

Watu 14 waliuawa na wengine 50 walijeruhiwa hapo jana katika hujuma ya kigaidi ya mripuko wa bomu uliotokea kwenye kituo cha treni ya chini ya ardhi cha Tekhnologichesky Institut mjini St. Petersburg nchini Russia.

Duru za usalama za Russia zimetangaza leo kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliyehusika na shambulio hilo la jana ni Akbarjon Djalilov, kijana wa miaka 22 mwenye asili ya Kyrgyzstan.../

Tags