Kufichuliwa hatua za kijasusi za Uturuki nchini Ujerumani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27386-kufichuliwa_hatua_za_kijasusi_za_uturuki_nchini_ujerumani
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa serikali ya nchi hiyo inawachunguza washukiwa ishirini wa Uturuki wanaotuhumiwa kufanya ujasusi na vitendo vilivyo nyuma ya pazia kwa maslahi ya serikali ya Uturuki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2017 22:03 UTC
  • Kufichuliwa hatua za kijasusi za Uturuki nchini Ujerumani

Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa serikali ya nchi hiyo inawachunguza washukiwa ishirini wa Uturuki wanaotuhumiwa kufanya ujasusi na vitendo vilivyo nyuma ya pazia kwa maslahi ya serikali ya Uturuki.

Inaonekana kuwa baada ya kuripotiwa suala hilo na vyombo vya habari, hivi sasa tunapasa kushuhudia mikwaruzano mipya katika uhusiano wa Ujerumani na Uturuki. Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Shirikiko la Ujerumani ilitangaza mwezi Machi mwaka huu kuwa imeanza kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya washukiwa hao wa ujasusi raia wa Uturuki. Vyombo vya habari vya Ujerumani wakati huo vilitangaza kuwa Shirika la Ujasusi la Uturuki (MIT) ndilo linalolengwa katika uchunguzi huo. Shirika hilo linatuhumiwa kuwafanyia ujasusi wafuasi wa Fethullah Gulen mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki. Gulen ambaye anatuhumiwa na Ankara kuwa alipanga njama ya mapinduzi iliyoshindwa mnamo mwezi Julai mwaka jana anaishi Marekani. Polisi ya Ujerumani mwezi Februari mwaka huu pia ilivamia makazi ya wanazuoni wanne wa Uturuki wanaotuhumiwa kuwajasusi wafuasi wa Gulen kwa maslahi ya serikali ya Uturuki. 

Fethullah Gulen, mpinzani mkuu wa rais wa Uturuki 

Uhusiano wa Uturuki na Ujerumani umeingia katika hali ya mivutano hivi sasa kwa kuzingatia hitilafu zilizopo kati ya pande mbili hizo. Hitilafu hizo zimeshtadi hasa kuhusiana na  kufanyika kura ya maoni ya marekebisho ya katiba huko Uturuki na vile vile kufuatia hatua ya serikali ya Ujerumani ya kuwazuia raia wa Uturuki wanaoishi Ujerumani kufanya mikutano yao sambamba na kuwazuia viongozi wa Uturuki kushiriki kwenye mijumuiko hiyo. Suala hilo limempelekea Erdogan kutoa radiamali kali ambapo katika matamshi yasiyo ya kawaida, Rais huyo wa Uturuki alizituhumu Ujerumani na nchi kadhaa za Ulaya kuwa zinatekeleza muamala unaofana na wa zama za Manazi. Mwanzoni mwa mwezi huu pia rais wa Uturuki aliituhumu serikali ya Ujerumani kuwa inatekeleza miamala ya kifashisti na kwamba inaunga mkono ugaidi kufuatia hatua ya serikali ya Berlin ya kufuta mikutano ya uchaguzi iliyoandaliwa kwa lengo la kuwakusanya raia wa Uturuki  milioni moja na laki tano wanaoishi Ujerumani; ambao wana haki ya kushiriki katika kura ya maoni yenye lengo la kumuongezea mamlaka Rais Recep Tayyep Erdogan. 

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki  

Pamoja na hayo yote, kufichuliwa hatua hizo za kijasusi za Uturuki nchini Ujerumani na kusahiliwa raia kadhaa wa Uturuki katika uwanja huo, huenda kukazidisha ufa na hitilafu kati ya Berlin na Ankara. Kadhia hii inaonyesha namna oparesheni ya Shirika la Ujasusi la Uturuki ilivyokuwa kubwa sana huko Ujerumani kulinganisha na tetesi zilizokuwa zikitolewa huko nyuma. Hasa ikizingatiwa kwamba lengo la oparesheni  hiyo ya kijasusi lilikuwa ni kupata taarifa kuhusu wafuasi wa Gulen na shughuli wanazofanya huko Ujerumani.  Berlin kwa upande wake inaona kuwa, hatua iliyochukuliwa na Ankara si ya kirafiki na inakinzana na maslahi ya taifa la Ujerumani. Hata hivyo ilitazamiwa kuwa, mara hii kama ilivyokuwa huko nyuma, serikali ya Ankara na hasa Rais Erdogan wa Uturuki angeishambulia kwa maneno na kuituhumu serikali ya Ujerumani  na kuituhumu kuwa inaeneza tuhuma za uwongo dhidi ya serikali ya Ankara. Hasa ikitiliwa maaani kwamba, serikali ya Ujerumani miezi kadhaa iliyopita ilikosoa pakubwa ubinywaji wa uhuru wa magazeti na ule wa kujieleza na pia kuhusu hali ya waandishi habari huko Uturuki  kukiwemo kutiwa mbaroni mwandishi habari wa Kijerumani raia wa Uturuki  kwa jina la Deniz Yucel anayefanya kazi katika gazeti la Die Welt la nchini Ujerumani. Kwa utaratibu huo, katika hali ambayo mivutano baina ya Ujerumani na Uturuki hadi sasa inahusishwa na baadhi ya mambo kama vile kufanyiwa marekebisho muundo wa kisiasa wa Uturuki, utawala wa sheria, kuheshimiwa misingi ya haki za binadamu na namna ya kuamiliana na wapinzani na vyombo vya habari; masuala ambayo yamesababisha kukosolewa serikali ya Erdogan, hivi sasa kitendo cha Shirika la Ujasusi la Uturuki cha kueneza ujasusi wake nchini Ujerumaini pia limejumuishwa katika orodha ya hitilafu kati ya Berlin na Ankara.