40 wapoteza maisha katika mafuriko Iran, Kiongozi Muadhamu atoa kauli
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27838-40_wapoteza_maisha_katika_mafuriko_iran_kiongozi_muadhamu_atoa_kauli
Makumi ya watu wamepoteza maisha katika janga la mafuriko kwenye mikoa ya kaskazini magharibi mwa Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 16, 2017 07:23 UTC
  • 40 wapoteza maisha katika mafuriko Iran, Kiongozi Muadhamu atoa kauli

Makumi ya watu wamepoteza maisha katika janga la mafuriko kwenye mikoa ya kaskazini magharibi mwa Iran.

Esmaeel Najjar, Mkuu wa Idara ya Kushughulikia Majanga ya Iran amesema watu 40 wameaga dunia kutokana na janga hilo la kimaumbile, lililosababishwa na mvua zinazonyesha katika mikoa ya kaskazini magharibi mwa nchi tokea Ijumaa iliyopita, ambapo mito imevunja kingo zake na kusomba nyumba pamoja na magari.

Amesema katika eneo la Azar Shahr, mkoa wa Azerbaijan Mashariki, watu 17 wamekufa kwa kusombwa na mafuriko hayo, huku makumi ya wengine wakipoteza maisha katika mikoa ya Azerbaijan Magharibi, Kurdistan na Zanjan.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Shahin Fathi, Afisa wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran amesema watu 1,150 wameokolewa kutokana na janga hilo katika vijiji na miji 33 ya maeneo hayo.

Sanjari na kutoa mkono wa pole kwa familia na wahanga wa mafuriko hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ameyataka mashirika yote husika kufanya hima kuwaokoa manusura wa janga hilo. Amesema: "Mamlaka husika zichukue hatua za dharura kuwaokoa manusura wa janga hilo bila kupoteza wakati, ili kuwapunguzia machungu."