Wananchi wa Iran waandamana kumuunga mkono Sheikh Issa Qassim
Wananchi wa Iran leo wameandamana katika mikoa mbalimbali baada ya Swala ya Ijumaa na kutangaza himaya yao kwa Sheikh Issa Qassim mwanazuoni wa Bahrain anayekabiliwa na vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Miji mbalimbali ya Iran leo, ukiwemo mji mkuu Tehran imeshuhudia maandamano makubwa baada ya Swala ya Ijumaa ambapo waandamanaji mbali na kulaani vitendo vya ukandamizaji vya vyombo vya usalama vya Bahrain dhidi ya raia wa nchi hiyo, wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa nchji hiyo ambaye anashikiliwa korokoroni.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba picha za mwanazuoni huyo na wanaharakati wengine mashuhuri wa kisiasa wa Bahrain wameutaka utawala wa Alal Khalifa wa Bahrain ukomeshe vitendo vya ukandamizaji dhidi ya raia wanaopaza sauti za kutaka mageuzi ya uongozi na kuweko uadilifu.
Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi.
Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima sauti na cheche za moto wa malalamiko hayo umewatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa, vijana na raia wengine wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela. Siasa hizo za utumiaji mabavu za utawala wa Aal Khalifa zimeifanya Bahrain kuwa uwanja wa ukandamizaji na mbinyo dhidi ya raia.