Iran yalaani hujuma ya Kabul, idadi ya waliouawa yapindukia 80
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i29856-iran_yalaani_hujuma_ya_kabul_idadi_ya_waliouawa_yapindukia_80
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoutikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kuuwa makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
(last modified 2025-11-26T03:04:14+00:00 )
May 31, 2017 15:00 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya Kabul, idadi ya waliouawa yapindukia 80

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoutikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kuuwa makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kusimama na kumuunga mkono jirani yake Afghanistan kwa kila hali.

Amesema shambulizi la kigaidi sehemu yoyote ile, wakati wowote ule na nlinalofanywa na kundi lolote lile ni ukatili na ni jambo la fedheha linalofaa kulaaniwa kwa nguvu zote.

Qassemi amesema Iran itaendelea kuunga mkono juhudi za kupatiwa ufumbuzi migogoro ya ndani ya mataifa mengine kwa njia za kisiasa pasina kuingilia mambo ya ndani wa nchi za kieneo na kimataifa ambazo bbadhi yake zenyewe zinaunga mkono magenge ya kigaidi.

Miili ikitolewa kwenye vifusi katika shambulizi la Kabul

Mripuko huo wa bomu lililotegwa garini umetikisika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul asubuhi ya leo na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 80 na kuwajeruhi wengine 350.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Afghanistan bomu hilo limeripuka katika Medani ya Zanbaq karibu na ikulu ya rais na balozi za kigeni katikati mwa Kabul. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekiri kuhusika na shambulizi hilo.