Rais Rouhani: Iran na Syria zinashirikiana kuangamiza ugaidi
(last modified Fri, 09 Jun 2017 04:32:26 GMT )
Jun 09, 2017 04:32 UTC
  • Rais Rouhani: Iran na Syria zinashirikiana kuangamiza ugaidi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mapambano halisi na ya kweli dhidi ya ugaidi na kurejesha amani ya kudumu katika eneo la Mashaiki ya Kati ni lengo la pamoja la Iran na Syria.

Rais Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Syria, Bashar Assad. Amesema Iran, kama ilivyokuwa huko nyuma, itaendelea kushirikiana na taifa la Syria katika mapambano dhidi ya ugaidi na kusisitiza kuwa, serikali na taifa la Iran litaendelea kuwa pamoja na watu wa Syria hadi utakapopatikana ushindi kamili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameeleza matumaini ya kudumishwa usitishaji vita nchini Syia ambao ni matokeo ya ushirikiano wa Iran, Syria na Russia na kusema kuwa, mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Marekani dhidi ya jeshi la Syria ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na yanapaswa kulaaniwa. Amesisitiza kuwa, mashambulizi hayo yanaonesha kuwa, madai yanayotolewa na Marekani kuhusu kupambana na ugaidi hayana msingi wowote. 

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Kwa upande wake Rais Bashar Assad wa Syria ametoa mkono wa pole kwa serikali na taifa la Iran kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika juzi mjini Tehran na kulaani ugaidi unaofanyika katika maeneo mbalimbali duniani.