Interpol yawakamata magaidi 37 Afrika Mashariki
Polisi ya Kimataifa (Interpol) imesema washukiwa 37 wa ugaidi, wakiwemo kadhaa wanaoaminika kuwa wanachama wa ISIS, wamekamatwa katika kanda ya Afrika Mashariki katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Interpol yenye makao yake makuu nchini Ufaransa, imesema leo Jumatatu kuwa, washukiwa hao wa ugaidi walikamatwa mnamo Novemba na Disemba 2024, wakati wa operesheni zilizofanywa kwa pamoja na shirika la polisi la Afrika Afripol.
Interpol imesema operesheni hizo barani Afrika zimepelekea kutiwa mbaroni watu 17 wakiwemo wawili wanaoshukiwa kuwa wanachama wa ISIS nchini Kenya; na vile vile kukamatwa kwa mshukiwa wa kundi la ISIS raia wa Msumbiji huko nchini Tanzania. Magaidi wengine walikamatwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia.
Cyril Gout, afisa wa Interpol amesema, "Mazingira tata ya Afrika Mashariki, kukosekana utulivu wa kisiasa, mipaka iliyo wazi, na changamoto za kijamii na kiuchumi, zinaendelea kuweka mazingira ya kufanya shughuli na harakati za kigaidi zishamiri."
Gout ameeleza bayana kuwa, "Matokeo haya mazuri (ya kukamatwa magadi 37) yanaonyesha nguvu ya ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi."