Khatibu: Siku ya Kimataifa ya Quds imeiletea Iran heshima
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kushiriki kwa wingi taifa la Iran katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, ni jambo ambalo limeuletea heshima na izza mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Sayyed Ahmad Khatami katika hotuba zake za sala ya Ijumaa wiki hii Tehran sambamba na kuwashukuru wananchi wa matabaka yote Iran kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, amesema ushiriki huo unaonyesha mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu mbele ya madola ya kiistikbari duniani.
Amesema kuchukizwa na uistikbari wa kimataifa na kupinga dhulma ni nukta zilizojitokeza wazi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran. Ameongeza kuwa, dola la Marekani ni la kitaghuti na kuongeza kuwa, athari mbaya za dola hilo la kibeberu na kiistikbari zinazonekanaa katika ulimwengu wa Kiislamu hasa nchini Yemen, Bahrain, Syria na nchi zingine za Kiislamu.

Amesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni nembo za uistikbari wa kimataifa na kuongeza kuwa, "Inasikitisha kuwa baadhi ya nchi za eneo kama vile Saudi Arabia zimejiunga na duara hilo la uistikbari."
Khatibu wa sala ya Ijumaa Tehran pia ameashiria oparesheni ya makombora ya Juni 18 iliyotekelezwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran dhidi ya ngome za magaidi wa ISIS au Daesh nchini Syria na kusema: "Ujumbe wa hujuma hiyo kwa Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao katika eneo ni huu kuwa, katika suala la kulinda usalama wake, Iran iko imara na wala haitalegeza msimamo. Akiashiria vikwazo vipya vya Bunge la Senate la Marekani dhidi ya Iran, Ayatullah Khatami amesema Iran itaendelea na mpango wake wa kuunda makombora na kusema vikwazo hivyo ni ishara kuwa Marekani haiwezi kuaminika.