Velayati: Mataifa ya eneo hili hayatasalimu amri mbele ya misimamo mikali
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema kuwa, mataifa ya eneo hili hayatasalimu amri mbele ya matakwa ya mirengo yenye misimamo mikali na waungaji mkono wao.
Ali Akbar Veleyati ameongeza kuwa, kunapaswa kuwepo ushirikiano na uratibu wa kimataifa sambamba na azma na irada ya kweli ili kukabiliana na mirengo yenye misimamo ya kufurutu ada, ile ya kitakfiri na makundi ya kigaidi katika kusimamia na kuendesha masuala ya eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini. Dakta Velayati ameyasema hayo hapa Tehran katika mazungumzo na Christian Masset, Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran ameeleza kuwa, baadhi ya nchi zinanufaika na hali ya mvutano na mgogoro iliyopo hivi sasa katika eneo hili la Mashariki ya Kati na hazitaki kuona amani na utulivu unadumishwa kwenye eneo hili muhimu. Dakta Velayati ameongeza kuwa, Iran itasimama imara kukabiliana na njama yoyote ya kutaka kuzidhoofisha na kuzigawa nchi za Mashariki ya Kati na inataka kulindwa umoja wa ardhi na kujitawala nchi zote za eneo hili ikiwa ni msingi mkuu wa siasa zake.
Vile vile ameshiria kuchaguliwa Emmanuel Macron kuwa Rais wa Ufaransa na akasema, anataraji kujitokeza matukio chanya kati ya nchi mbili za Iran na Ufaransa kufuatia kuingia madarakani rais mpya huko Ufaransa. Ameongeza kuwa, Iran iko tayari kushirikiana na Ufaransa katika jitihada za kurejesha amani na utulivu duniani.
Naye Christian Masset Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa amesema kuwa, nchi mbili za Iran na Ufaransa zina uhusiano wa kihistoria na wa kiutamaduni wa siku nyingi na kwamba pande mbili zinaweza kutumia nyanja hizo kukuza ushirikiano kati yao. Masset ameashiria vile vile kiwango cha uhusiano wa kibiashara kati ya Tehran na Paris na kueleza kuwa, uhusiano wa Iran na Ufaransa hivi sasa umeongezeka kwa asilimia 400 na hilo limeandaa fursa nyingi nzuri za kiuchumi katika nyanja mbalimbali.