Qassemi: Palestina bado ni kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa kuendelea ukandamizaji mkubwa na kukiukwa haki za raia wa Palestina katika kufikia maeneo matukufu huko Quds Tukufu kunaonyesha kuwa Palestina iliyodhulumika ingali kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Bahram Qassemi amelaani kuendelea kukandamizwa wananchi madhlumu wa Palestina huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuzuiwa kuingia katika Msikiti wa al Aqsa kwa ajili ya sala na kueleza kuwa fikra za waliowengi, vyombo vya habari, wanafikra huru, mataifa na serikali mbalimbali wanapasa kuwaunga mkono raia wa Palestina wanaodhulumika mbele ya uvamizi na vitendo visivyo vya kibinadamu vya Wazayuni maghasibu.
Qassemi ameitaja Quds Tukufu na Miskiti wa Aal Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu kuwa ni milki ya milele ya Waislamu wote duniani na wananchi wa Palestina na kuongeza kuwa utawala wa Kizayuni unatekeleza vitendo hivyo vya kujitanua na ukandamizaji kama chimbuko na chanzo cha ugaidi wa kiserikali katika eneo hilo.
Qassemi amekosoa kimya cha baadhi ya nchi za eneo zinazojiiita kuwa ni za Kiislamu na kitovu cha Ulimwengu wa Kiislamu na kuzitolea wito taasisi za kimataifa khususan Umoja wa Mataifa kusimama imara na kuchukua hatua mkabala na hatua za ukandamizaji na siasa za ubaguzi wa kijamii na kimadhehebu zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni.
Utawala huo umewawekea vizuzizi raia wa Palestina na kuwazuia kuingia katika msikiti wa al Aqsa tangu tarehe 14 mwezi huu ikiwa ni katika kuendelea kwa vitendo vya mabavu na ukandamizaji vya utawala huo dhidi ya Wapalestina.