Iran: Yaishitaki Marekani kwa hatua yake ya kuiwekea vikwazo vipya Tehran
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran sambamba na kubainisha kwamba, ukiukaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA uliofanywa na Marekani uko wazi, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislam ya Iran imewasilisha mashitaka kwenda kwa baraza na kamisheni inayosimamia makubaliano hayo, kutokana na hatua ya Washington ya kuliwekea taifa hili vikwazo vipya.
Ali Larijani ameyasema hayo leo mjini Qum, kusini mwa mji wa Tehran mbele ya waandishi wa habari ambapo sambamba na kuashiria kikao cha kamati ya uangalizi wa makubaliano hayo ya JCPOA cha Iran amesema, Tehran imeazimia vilivyo kuizuia Marekani kufikia malengo yake. Ameongeza kuwa, baadhi ya nchi zimetangaza wazi kwamba hatua hiyo mpya ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahesabiwa kuwa ni ukiukaji usio na shaka wa moyo wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.
Sambamba na kufafanua kuwa Wamarekani wanajaribu kuzuia utekelezwaji wa makubaliano hayo ya nyuklia, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amesema, maamuzi ya Kongresi ya Marekani katika kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran hayana lengo jingine ghairi ya kuzuia anga ya uwekezaji ndani ya Iran. Katika kikao cha Jumatatu ya jana, kamati ya Uangalizi ya Iran inayosimamia utekelezwaji wa makubaliano hayo kilichosimamiwa na Rais Hassan Rouhani, kulisisitiziwa juu ya kutolewa jibu kali kabisa kuhusiana na hatua hiyo ya kiuhsama ya Marekani dhidi ya nchi hii. Wiki iliyopita, Konresi ya Marekani ilipasisha vikwazo mpya dhidi ya Iran ya Kiislamu hatua ambayo imekosolewa na pande mbalimbali za dunia.