Araqchi: Vikwazo vipya vya US vinalenga kuisambaratisha JCPOA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kusaini sheria ya vikwazo vipya dhidi ya Tehran ni njama ya Washington ya kutaka kusambaratisha makubaliano ya nyuklia ya Vienna yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.
Sayyid Abbas Araqchi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa aliyasema hayo jana, muda mfupi baada ya Trump kusaini kuwa sheria muswada wa vikwazo vipya dhidi ya Tehran.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu mwafaka na lenye mantiki kutokana na hatua hiyo ya kiuhasama ya Marekani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Iran inataraji kuwa nchi zinazounda kundi la 5+1 zina wajibu wa kuheshimu na kutekeleza ahadi zao kuhusiana na JCPOA.
Licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kusaini kuwa sheria mpango wa vikwazo uliopitishwa na Bunge la Wawakilishi na Seneti ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Korea Kaskazini, lakini ameeleza kupitia taarifa wasiwasi alionao kuhusu athari hasi zinazoweza kutokea kutokana na hatua hiyo.
Tayari Jamhuri ya Kiislam ya Iran imewasilisha malalamiko yake kamisheni inayosimamia makubaliano hayo, kutokana na hatua ya Washington ya kuliwekea taifa hili vikwazo vipya.