Iran na Uturuki zajadili kuimarisha uhusiano wa kiulinzi
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Uturuki mjini Ankara, kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiulinzi wa pande mbil
Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara baada ya mkutano wake na Rais wa Uturuki, Recep Teyyip Erdogan kuwa, masuala ya kieneo na kupambana na zimwi la ugaidi ni katika mambo waliyoyazungumza katika mkutano wao wa faragha.
Kuhusu ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi, Meja Jenerali Baqeri amesema: "Pande mbili zimekubaliana kuhusu kuwa na ushirikiano kwa kubadilishana elimu, wanafunzi sanjari na kuwa na kozi za pamoja za masuala ya kiulinzi."
Kadhalika amesema Tehran na Ankara zimekubaliana kuimarisha mabadilishano ya taarifa katika uga wa kukabiliana na ugaidi.
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Iran na Uturuki kwa pamoja zimeafikiana kuwa, kufanyika kura ya maoni ili eneo la Kurdistan lijitenge na Iraq wakati huu kunaweza kuzidisha taharuki nchini Iraq na katika nchi jirani.
Kabla ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Erdogan hapo jana, Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Uturuki, Jenerali Hulusi Akar na wawili hao wakazungumzia namna ya kuimarisha usalama wa nchi mbili hizo hususan katika maeneo ya mipakani na kuimarisha jitihada za kupambana na ugaidi.
Kadhalika amekutana na kufanya mazungumzo na Nurettin Canikli. Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, na pande mbili zikajadili umuhimu wa nchi za Mashariki ya Kati kubuni sera ya pamoja inayopinga uingiliaji wa masuala ya ndani ili kudhamini usalama, amani na uthabiti katika eneo hili.