Larijani: Migogoro ya nchi za Kiislamu, sababu ya kusahauliwa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33935-larijani_migogoro_ya_nchi_za_kiislamu_sababu_ya_kusahauliwa_palestina
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, nchi nyingi za Kiislamu hivi sasa zina migogoro ya ugaidi na ya kiusalama, jambo ambalo limepelekea baadhi ya wanasiasa waisahau kadhia ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2017 22:06 UTC
  • Larijani: Migogoro ya nchi za Kiislamu, sababu ya kusahauliwa Palestina

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, nchi nyingi za Kiislamu hivi sasa zina migogoro ya ugaidi na ya kiusalama, jambo ambalo limepelekea baadhi ya wanasiasa waisahau kadhia ya Palestina.

Ali Larijani alisema hayo jana (Jumatatu) mbele ya wafanyakazi wa bunge la Iran na kuongeza kuwa, baadhi ya nchi za eneo hili na nje yake zimeshughulishwa na siasa za kujaribu kuifanya Iran itengwe ili baadaye zisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu imetengwa kutokana na misimamo yake kuhusu Palestina, Syria, Yemen, Bahrain na vita dhidi ya ugaidi, hata hivyo zimeshindwa.

Watoto wa Ghaza, Palestina wakiteka maji ya mgao katika vifusi vya nyumba na misikiti iliyobomolewa kwa mabomu katika mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni

 

Ameongeza kuwa, mabadiliko yaliyotokea katika serikali ya Marekani na matamshi ya rais wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya Iran yamekuwa yakilenga kuifanya Iran itengwe kimataifa. Hata hivyo hatua ya wananchi wa Iran ya kujitokeza kwa wingi sana katika uchaguzi wa rais wa tarehe 19 Mei 2017 ilitoa jibu madhubuti kwa siasa hizo mbovu za Marekani.

Spika wa Bunge la Iran pia amesema: Tehran imechukua msimamo wa wazi kuhusiana na jinai za miezi ya hivi karibuni walizofanyiwa Waislamu wa Myanmar mbele ya kimya cha kutisha cha jamii ya kimataifa. Aidha mara kwa mara Iran imekuwa ikitangaza msimamo wake kuhusiana na matukio ya Yemen, Syria na Bahrain jambo ambalo linaonesha namna Iran ilivyo imara wakati wote katika medani mbalimbali.

Vile vile amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijabadilisha misimamo yake, wakati nchi nyingine nyingi za eneo hili zinabadilisha mara kwa mara misimamo yao kwa ajili ya kuyaridhisha madola ya kibeberu.