Zarif: Iran haina imani na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34955-zarif_iran_haina_imani_na_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA haukufikiwa kwa msingi wa kuaminiana na kimsingi Iran haina imani na Marekani.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 28, 2017 04:30 UTC
  • Zarif: Iran haina imani na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA haukufikiwa kwa msingi wa kuaminiana na kimsingi Iran haina imani na Marekani.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika kituo cha utafiti cha Marekani cha Klabu ya Asia mjini New York na katika mahojiano na mtangazaji maarufu wa Marekani Charlie Rose.

Amesema, hivi sasa Marekani inapaswa itangaze uamuzi wake kuhusu JCPOA ili kuonyesha kama jamii ya kimataifa inaweza kuwa na imani na Washington au la.

Dakta Zarif ameashiria kwamba Iran haijakiuka makubalinao yoyote ya kimataifa na wala haihitaji kuwekewa vizuizi zaidi na kubainisha kwamba, Iran haiitakidi kama silaha za nyuklia zina manufaa kwa usalama wake wa taifa na kwamba endapo Marekani itajitoa kwenye makubaliano ya JCPOA itachukua maamuzi yanayostahiki kulingana na mazingira.

Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 zilipofikia makubaliano ya JCPOA

Katika mahojiano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza pia kwamba ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wapinzani na mgogoro kati ya Qatar na Saudi Arabia ni matokeo ya siasa ghalati za Rais Donald Trump wa Marekani katika Mashariki ya Kati na kuongeza kwamba eneo la Mashariki ya Kati linahitaji wito wa mazungumzo.

Zarif ameashiria pia siasa mbovu za Saudia kuhusiana na Yemen na Syria na kueleza kwamba Saudia Arabia ambayo ni mmoja wa wadau muhimu katika eneo inatakiwa iachane na njozi ya kuiweka kando Iran katika Mashariki ya Kati kwa sababu kudhamini usalama wa eneo hili kunahitaji ushirikiano.

Amesema kinyume na Saudia, njia ya ufumbuzi iliyopendekezwa na Iran kwa ajili ya kutatua migogoro ya Yemen na Syria ni kutekelezwa usitishaji vita, kufikishwa misaada ya kibinadamu, kufanyika mazungumzo ya kisiasa na kufanyika uchaguzi kwa ajili ya kuunda serikali jumuishi katika nchi hizo.../