Onyo la Zarif kuhusiana na kujiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35045-onyo_la_zarif_kuhusiana_na_kujiondoa_marekani_katika_makubaliano_ya_jcpoa
Misimamo ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani inathibitisha wazi kwamba rais huyo hayuko tayari kukubali kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake za mapatano ya nyuklia yanayojulikana kwa ufupi kama JCPOA licha ya nchi za Ulaya na hata wanasiasa mashuhuri wa nchi yake mwenyewe kuthibitisha suala hilo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 30, 2017 08:48 UTC
  • Onyo la Zarif kuhusiana na kujiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA

Misimamo ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani inathibitisha wazi kwamba rais huyo hayuko tayari kukubali kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake za mapatano ya nyuklia yanayojulikana kwa ufupi kama JCPOA licha ya nchi za Ulaya na hata wanasiasa mashuhuri wa nchi yake mwenyewe kuthibitisha suala hilo.

Misimamo hiyo imebainika wazi kiasi cha kumfanya Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atabiri katika mazungumzo yake na magazeti ya Guardian na Financial Times kwamba, Trump hivi karibuni atatekeleza tishio lake la kujiondoa katika makubaliano hayo, atakapowasilisha ripoti yake kuhusiana na suala hilo katika Congress ya nchi hiyo hapo tarehe 15 mwezi ujao wa Oktoba, ambapo atakataa kuthibitisha kwamba Iran imetekeleza mapatano hayo. Katika mahojiano yake na mageti mawili yaliyotajwa, Zarif amezitaka nchi za Ulaya kuipuuza Marekani iwapo Trump atachukua hatua hiyo ya upande mmoja ya kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa ambayo yalichukua miaka mingi kufikiwa. Amesema iwapo nchi za Ulaya zitaiga mfano wa Marekani kwa kujitoa kwenye mapatano hayo ni wazi kuwa yatakuwa yamevunjika na hivyo kuipa Iran fursa ya kuendelea kufikia kiwango cha juu kabisa cha teknolojia ya nyuklia, ambacho kilikuwa hakijafikiwa kabla ya kufikiwa mapatano ya JCPOA mwaka 2015.

Donald Trump anayetaka kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA

Ni wazi kuwa kama Trump atakwepa kuthibitisha kufungamana Iran na mapatano hayo katika ripoti yake ya tatu kwa Congress ambayo imepangwa kuwasilishwa hapo tarehe 15 Oktoba, Congress itakuwa na fursa ya siku 60 kuanza kutekeleza tena vikwazo vilivyosimamishwa vya nyuklia dhidi ya Iran. Kama alivyosema Zarif iwapo vikwazo hivyo vitatekelezwa, basi Iran nayo haitalazimika kutekeleza wala kufungamana na mapatano ya JCPOA. Kama Trump atachukua hatua ya kukanyaga na kuyapuuza mapatano hayo ni wazi kuwa Iran itakuwa na machaguo mengine mengi ya kukabiliana na suala hilo. Miongoni mwa machaguo ya haraka ni Iran kuanzisha tena shughuli zake za nyuklia zinazotekelezwa kwa malengo ya amani ambazo zilisimamishwa kufuatia mapatano ya JCPOA. Utafiti na ustawi katika nyanja za nyuklia umeiwezesha Iran kufikia teknolojia mpya na ya kisasa kabisa hivyo iwapo italazimika, Iran itatekeleza ipaswavyo machaguo iliyonayo katika uwanja huo ili kukabiliana na hatua haribifu za Trump dhidi ya mapatano ya kimataifa ya JCPOA.

Nchi zilizotia saini mapatano ya JCPOA

Chaguo jingine la Iran katika kujibu hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mapatano hayo ni Tehran pia kujiondoa kwenye mapatano hayo. Iran bado ina machaguo mengine mengi na kila moja litatekelezwa kwa mujibu wa hatua zitakazochukuliwa na kundi la 5+1 kufuatia uamuazi wa Marekani wa kupuuza na kujiondoa katika mapatamo hayo. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, iwapo nchi za Ulaya, Russia na China zitachukua uamuzi wa kuifuata Marekani kwa kujitoa kwenye mapatano hayo kwa madhara ya Iran, ni wazi kuwa mapatano hayo yatachukuliwa kuwa yamekufa. Kwa kutilia maanani misimamo na matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na nchi za Ulaya, Russia na China katika kuunga mkono mapatano ya JCPOA inaonekana kuwa Marekani itaachwa peke yake katika njia ya kujiondoa katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa. Kuhusiana na suala hilo, John Kerry, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekan, katika makala aliyoandika hivi karibuni katika gazeti la Washington Post ametahadharisha kwamba Marekani itawapoteza  washirika wake wa Ulaya iwapo itachukua uamuzi wa kutaka kujitoa kwenye mapatano hayo na kwamba suala hilo linatoa ujumbe kwamba inalazimika kutekeleza ahadi zake.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Katika upande wa pili, huku akisisitiza nukta hii kwamba Iran daima imekuwa ikitekeleza ahadi na majukumu yake kuhusiana na mapatano ya JCPOA, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya pia alisema hivi karibuni kwamba umoja huo utafanya kila linalowezekana ili kulinda mapatano ya JCPOA hata kama Marekani itachukua uamuzi wa upande mmoja wa kujitoa katika mapatano hayo ya kimataifa. Taasisi pekee ya kimataifa ambayo ina jukumu la kuthibitisha iwapo Iran imefungamana na mapatano hayo au la ni Wakala wa Kiamaifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA ambapo kufikia sasa umethibitisha kupitia ripoti zake saba kwamba Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na mapatano hayo. Kwa msingi huo si mitizamo wala malengo binafsi ya Donald Trump yanapaswa kuchukuliwa kuwa kipimo cha kujua iwapo Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu na JCPOA au la. Hivyo basi hatua yoyote itakayochukuliwa na Trump kwa ajili ya kuvuruga mapatano hayo ya kimataifa kwa mara nyingine itaibua kashfa na kuanika wazi mbele ya macho ya walimwengu, tabia ya kuchukiza ya nchi hiyo kukiuka mara kwa mara ahadi zake kwa jamii ya kimataifa.