Iran itatumia fursa iliyoibuliwa na uhasama wa Rais wa Marekani kuijiimarisha kijeshi
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, IRGC, amesema Iran itatumia fursa iliyojitokeza katika matamshi yaliyojaa uhasama ya Rais wa Marekani kujiimarisha kijeshi.
Meja Jenerali Mohammad Ali Jaafari Kamanda wa IRGC akizungumza katika kikao cha Baraza la Kistratijia la IRGC ameonya kuwa, iwapo Marekani itatekeleza sheria ya vikwazo vya kukabiliana na mahasimu wake inayojulikana kama Countering America’s Adversaries Through Sanctions Act (CAATSA) basi Washington inapaswa kuviweka vituo vyake vya kijeshi nje ya duara la kilomota elfu mbili kutoka Iran ambao ni umbali yanayoweza kufika makombra ya Iran.
Agosti pili Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini sheria hiyo ya CAATSA baada ya kupitishwa katika bunge la nchi hiyo. Sheria hiyo inaiwezesha serikali ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi.
Meja Jenerali Jaafari aidha ameonya kuwa iwapo Marekani italiwekea vikwazo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kulitaja jeshi hilo kuwa eti ni kundi la kigaidi, basi jeshi hilo litawatazama wanajeshi wa Marekani kote duniani hasa Mashariki ya Kati kuwa ni sawa na kundi la kigaidi la ISIS na kuwalenga.
Meja Jenerali Jaafari ameongeza kuwa, Marekani inafuata mkondo ghalati kabisa kuhusu masuala ya eneo. Aidha amesema iwapo Marekani inaibua uzushi kuhusu Iran ili kuilazimu nchi hii iketi kwenye meza ya mazungumzo inafanya kosa kubwa.
Kamanda wa IRGC amesema vikwazo vipya vya Marekani vitafunga daima mlango wa maelewano na kwamba vitakamilisha uzoefu wa Iran katika mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA. Amesema Marekani imekuwa ikifuatilia mazungumzo si kwa ajili ya kutatua matatizo bali kwa ajili ya kuyatumia kama chombo cha kuendeleza uhasama wake dhidi ya Iran.