Zarif: Iran inataka suluhu, uthabiti na usalama katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35481-zarif_iran_inataka_suluhu_uthabiti_na_usalama_katika_eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kwa muda sasa eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na machafuko na ukosefu wa uthabiti baada ya vikosi vya kijeshi vya kigeni kuanza kuingilia masuala ya eneo hili na amesisitiza kwamba Tehran inataka suluhu, uthabiti na amani vitawale katika mataifa yote ya eneo hili.
(last modified 2026-02-12T09:09:48+00:00 )
Oct 10, 2017 16:50 UTC
  • Zarif: Iran inataka suluhu, uthabiti na usalama katika eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kwa muda sasa eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na machafuko na ukosefu wa uthabiti baada ya vikosi vya kijeshi vya kigeni kuanza kuingilia masuala ya eneo hili na amesisitiza kwamba Tehran inataka suluhu, uthabiti na amani vitawale katika mataifa yote ya eneo hili.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika makala yake iliyochapishwa katika toleo la leo la jarida la The Atlantic.

Huku akiashiria kwamba baadhi ya majirani wa Iran hawataki kuwepo na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati, Dakta Zarif amesema waitifaki wa Magharibi, badala ya kushughulikia masuala ya wananchi wao, wanautumia utajiri wao kununulia silaha, kueneza Uwahabi, kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kuvuruga amani katika eneo kwa kuishambulia kijeshi Yemen, kuingilia masuala ya ndani ya Bahrain na kuunga mkono Daesh (ISIS) katika nchi za Syria na Iraq.

Huku akiashiria kwamba baada ya makubaliano ya nyuklia majirani wa Iran wangeliweza kuwa na mabadilishano makubwa zaidi ya kibiashara na ya uwezekaji na Tehran lakini wakafanya kinyume chake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu amesema, baada ya makubaliano ya JCPOA baadhi ya majirani wamejaribu kujenga dhana hewa ya kujaribu kuonyesha kuwa Iran ndiyo chanzo kikuu cha kukosekana uthabiti.

Mfalme Salman wa Saudia ambaye nchi yake ni chanzo cha machafuko Mashariki ya Kati

Katika makala yake hiyo, Zarif ameashiria pia uwezo wa kiulinzi wa Iran na kueleza kwamba, kutokana na uadui wa baadhi ya majirani na kwa kuzingatia tajiriba na uzoefu wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baathi wa Iraq dhidi yake, Jamhuri ya Kiislamu imejitahidi kuhakikisha inaimarisha uwezo wake wa kiulinzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameeleza kwamba nchi au upande wowote ule hauna sababu ya kuhofu uwezo wa makombora na nguvu za kijeshi za Iran labda iwe na ndoto ya kushambulia au kufanya hujuma ya kigaidi dhidi ya Iran.../