Russia: Marekani itahatarisha usalama wa dunia ikijiondoa JCPOA
Russia imeonya kuwa Marekani itahatarisha usalama wa dunia ikijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran yaliyotiwa saini mwaka 2015 baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Taarifa mbalimbali zimemnukuu Dmitry Peskov, msemaji wa Rais Vladimir Putin wa Russia akizungumza hayo jana Ijumaa na kusema kuwa: 'Hatua yoyote ya Marekani dhidi ya mapatano ya nyuklia ya Iran itakuwa na matokeo mabaya sana." Aidha amesema hatua kama hiyo ya Marekani itahatarisha usalama wa dunia na mchakato wa kuangamzia silaha za nyuklia ulimwenguni. Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesema, nchi yake itaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya Iran.
Itakumbukwa kuwa Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilifikia mapatano kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran.
Mapatano hayo ambayo ni maarufu kwa jina la JCPOA yalifikiwa mwezi Julai 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 16 mwaka jana. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia huku nchi za Magharibi zikitakiwa ziiondolee Iran vikwazo.
Lakini pamoja na hayo Marekani inakaidi mapatano hayo huku Rais Donald Trump wa nchi hiyo akiyapinga waziwazi mapatano hayo.
Umoja wa wa Ulaya, Russia na China zimetangaza bayana kuwa zinaunga mkono mapatano hayo ya nyuklia na hivyo kumtenga rais wa Marekani.