Rais Rouhani: Azma ya Iran ni kustawisha uhusiano na Bara la Afrika
Rais Hassan Rouhani amesema kustawisha na kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika hasa Nigeria ikiwa ni nchi rafiki na ya Kiislamu ni miongoni mwa misingi ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kwamba mashirika makubwa ya Kiirani yako tayari kutekeleza miradi ya maendeleo nchini Nigeria.
Rais Rouhani ameyasema hayo wakati akipokea hati za utambulisho za Ibrahim Hamza, balozi mpya wa Nigeria hapa nchini. Ameongeza kuwa inapasa uwezo na fursa zilizopo katika nchi za Iran na Nigeria katika sekta mbalimbali zitumiwe kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa pande mbili.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia udharura wa kufanywa juhudi za kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Abuja na kueleza kwamba Iran iko tayari kutoa huduma za kiufundi na kiuhandisi katika sekta mbalimbali za ujenzi wa barabara, nishati na uzalishaji umeme nchini Nigeria na vilevile kustawisha uhusiano wa kiutamaduni, vyuo vikuu, wa kiteknolojia na wa kiuchumi na nchi hiyo.
Dakta Rouhani amezungumzia pia ulazima wa Iran na Nigeria kushirkiana katika jumuiya za kimataifa na akabainisha kwa kusema: leo ugaidi ni hatari kwa ulimwengu mzima, na kupambana nao kunahitaji irada na ushirikiano wa nchi zote.
Katika mazungumzo hayo, balozi mpya wa Nigeria hapa nchini Ibrahim Hamza, mbali na kukabidhi hati zake za utambulisho kwa Rais Rouhani ameashiria udharura wa kustawishwa uhusiano wa nchi mbili katika nyuga mbalimbali na kuelezea hamu ya nchi yake ya kupanua uhusiano na ushirikiano wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../