IAEA: Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Sun, 29 Oct 2017 15:53:47 GMT )
Oct 29, 2017 15:53 UTC
  • IAEA: Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Kwa mara nyingine tena Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) amesema kuwa Iran imefungamana na kutekeleza wajibu na majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Yukia Amano ambaye yuko katika safari rasmi ya kikazi hapa Tehran amesema hayo leo Jumapili katika kikao na waandishi wa habari, akiwa pamoja na Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI).

Mkuu huyo wa IAEA amebainisha kuwa, "Wakala huu unaamini kuwa, makubaliano ya JCPOA ni mafanikio muhimu ambayo yanafaa kuheshimiwa na kutekelezwa na kila upande."

Kwa upande wake, Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo wa kurutubisha urani hadi kiwango cha asilimia 20 ndani ya siku nne, lakini haitaki makubaliano ya JCPOA yavunjike.

Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa AEOI

Wakati huo huo, Behrouz Kamalvandi, Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran kadhia ya kukaguliwa vituo vya kijeshi vya Iran haipo katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 baina ya Iran na madola makuu sita duniani. Amesema kile ambacho IAEA inaweza kuomba ni kukagua vituo vya nyuklia vya Iran.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi kufikia sasa umethibitisha mara nane kwamba Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya nyuklia; huku Marekani iking'ang'ania kuwa Iran imekwenda kinyume na makubaliano hayo licha ya wakala wa IAEA kukagua mara kwa mara vituo vya nyuklia hapa nchini.