Iran na Ghana zasisitiza kupanua ushirikiano wao katika sekta ya kilimo
(last modified Wed, 15 Nov 2017 03:53:17 GMT )
Nov 15, 2017 03:53 UTC
  • Iran na Ghana zasisitiza kupanua ushirikiano wao katika sekta ya kilimo

Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran na Makamu wa Rais wa Ghana wamesisitizia udharura wa kufanyika kikao cha kamisheni ya pamoja ya uchumi na kupanuliwa ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya nchi mbili.

Mahmoud Hojjati, Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran yuko nchini Ghana akiongoza ujumbe wa watu 60 kutoka sekta za serikali na za binafsi kushiriki kikao cha sita cha kamisheni ya pamoja ya Iran na Ghana kinachofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Accra.

Katika mazungumzo aliyofanya na Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawumia hapo jana, Hojjati amesema Iran na Ghana zina uwezo na fursa nzuri za ushirikiano katika sekta za miundombinu, ujenzi wa mabwawa, ujenzi wa barabara, utengezaji dawa na huduma za tiba, mbolea za kemikali, utoaji mafunzo ya kiufundi na kitaalamu na utafiti wa kilimo.

Rais Hassan Rouhani akimlaki Rais wa zamani wa Ghana John Dramani Mahama alipotembelea Iran

Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran ameeleza kuwa Iran inaweza kuipatia Ghana uwezo na utaalamu wake katika sekta za ufundi na kilimo katika nyuga mbalimbali ikiwemo ya ukulima wa utumiaji mitambo, mbinu mpya za umwagiliaji maji na uboreshaji mazao ya kilimo.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Ghana Mahamudu Bawumia amekaribisha ushirikiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kustawisha ukulima wa utumiaji mitambo, kudhaminiwa mbolea za kemikali na chanjo za mifugo.../ 

Tags