Zarif: Saudia inachukua hatua za kijinga na kihasama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Wasaudia wanapuuza uhakika na hali halisi ya kihistoria na kuchukua hatua za kihasama na kijinga ambazo zinaendelea kuwasababishia madhara wao wenyewe.
Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akizungumzia siasa za kuzusha migogoro za mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na uwezekano wa kutokea vita baina ya Iran na Saudia, amesema kuwa, Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima zimejengeza kwa msingi wa mantiki, hekima na busara.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, badala ya kuzidisha machafuko na vita, Jamhuri ya Kiislamu inataka kuwepo amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Zarif ameashiria uharibifu unaofanywa na Saudia katika nchi za Syria, Yemen, Iraq na Lebanon na kusema: Watu wa eneo hili wamepata madhara mengi kutokana na sera hizo za watawala wa Riyadh na kuna ulazimishwa wa kusitishwa mwenendo huo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa Saudi Arabia inaendeleza makosa yake ya huko nyuma na yasiyo na tija na kusisitiza kuwa, Riyadh inapaswa kukubali hali halisi ya eneo la Mashariki ya Kati na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.