Mkutano wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran na kushirikisha nchi 70
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36921-mkutano_wa_umoja_wa_kiislamu_kufanyika_tehran_na_kushirikisha_nchi_70
Mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umepangwa kufanyika wiki ijayo katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran kwa kuhudhuriwa na wageni 250 kutoka nchi 70 duniani.
(last modified 2025-10-23T05:45:52+00:00 )
Nov 28, 2017 16:34 UTC
  • Mkutano wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran na kushirikisha nchi 70

Mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umepangwa kufanyika wiki ijayo katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran kwa kuhudhuriwa na wageni 250 kutoka nchi 70 duniani.

Akizungumza na waandishi habari hii leo mjini Tehran, Ayatullah Muhsin Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mkutano huo ambao utafanyika kuanzia Disemba 5-7 utawaleta pamoja wanazuoni, wanafikra na viongozi wa kisiasa kutoka nchi za Kiislamu wakiwemo mawaziri kadhaa.

Amesema kiwango cha ushiriki katika mkutano huo ni ishara kuwa ulimwengu wa Kiislamu una azma ya kukabiliana na madola ya kibeberu na kiistikbari na kuzima njama zao za kuibua mifarakano.

Ayatullah Araki pia ameashiria ushindi wa hivi karibuni wa mrengo wa muqawama na kusambaratishwa ngome ya kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS Syria na Iraq na kusema, kuwa, ushindi huo unaandaa mazingira ya mshikamano zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Imam Khomeini MA alipendekeza kuwepo Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Wakati huo huo mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Iran, IRIB, Mhandisi Ali Askari amesema shirika hilo lina nafasi muhimu katika kuleta umoja wa Kiislamu. Akizungumza baada ya mkutano na Ayatullah Muhsin Araki hii leo, Mhandisi Askari amesema kongamano la kimatiafa la Umoja wa Kiislamu ni hatua muhimu katika kuleta mshikamano baina ya Waislamu duniani ili waweze kukabiliana na maadui.

Mkutano huo wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal nao Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaitakidi tarehe hiyo kuwa ni 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha hitilafu ya wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.