Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Bila shaka Palestina itakombolewa tu
Ayatullah Ali Khamanei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja Marekani na utawala haramu wa Israel kuwa Mafirauni wa zama na dunia ya leo.
Akizungumza leo Jumatano mbele ya hadhara kubwa ya wakuu wa mihimili mitatu ya dola la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wakuu wa Mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na wageni wa Kongamano la Wiki ya Umoja wa Kiislamu kwa mnasaba wa kuzaliwa Mtume Mtukufu (saw) na Imam Jaffar Swadiq (as), Ayatullah Khamenei ameashiria juhudi kubwa zinazofanywa na Mafirauni wa zama kwa ajili ya kuzua hitilafu na vita kati ya Umma wa Kiislamu na kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wa Marekani wamekiri ima kwa kujua au kutojua kwamba vita na mapigano yanapaswa kuanzishwa katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ili kuuandalia usalama utawala wa Kizayuni na hivyo kuufanya uzuie kupatikana maendeleo yoyote katika ulimwengu wa Kiislamu ambao kwa sasa unaoshuhudia umwagikaji mkubwa wa damu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba kwa hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatumia lugha ya nasaha kuwanasihi vibaraka wa Marekani katika eneo, na kuwa haina nia yoyote ya kujibu matamshi ya baadhi ya majahili, lakini kwamba la muhimu kwa sasa ni kuwanasihi wasiwahudumie madhalimu kwa sababu watadhurika wao wenyewe kama inavyothibitisha hilo Qur'ani Tukufu kwamba wanaoshirikiana na madhalimu hatimaye wataangamia tu.
Hali inayotawala sasa katika eneo na hasa katika nchi za Kiislamu na hasa kuhusiana na suala la Palestina na Quds Tukufu, inahitajia uzingatiaji maalumu wa serikali za Kiislamu kuhusu masuala mawili ambayo ni Umoja wa Kiislamu na mapambano, kuliko wakati mwingine wowote ule. Sambamba na kutekelezwa njama za makundi ya kitakfiri ya Kiwahabi na Kizayuni katika nchi za Kiislamu za Syria na Iraq, baadhi ya nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia ziliamua kushirikiana kwa karibu na maadui sugu wa Umma wa Kiislamu kwa shabaha ya kulinda maslahi ya Marekani na Wazayuni katika eneo. Kuboreshwa uhusiano wa watawala wasiopenda mageuzi wa Kiarabu na utawala haramu wa Israel bila shaka ni njama mpya inayotekelezwa na Marekani kwa lengo la kuufanya ulimwengu wa Kiislamu usahau kabisa kadhia ya Palestina. Juhudi zinazofanywa hivi sasa na Marekani kwa ajili ya kuuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu na kuutambua rasmi mji huo mtakatifu kuwa ni mji mkuu wa utawala huo wa Kizayuni kwa hakika ni njama inayotokana na ushirikiano wa karibu wa Mafirauni wa zama. Rais Donald Trump wa Marekani anatazamiwa kutangaza rasmi msimamo wake kuhusiana na suala hilo leo Jumatano.
Kuhusu hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Madai ya maadui wa Uislamu kuhusu kutangazwa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, yanatokana na kushindwa kwao na bila shaka ulimwengu wa Kiislamu utakabiliana vilivyo na njama hiyo na Wazayuni kupata pigo kubwa zaidi, ambapo bila shaka hatimaye Palestina itakombolewa.
Quds na Suala la Palestina ni muhimili wa nguvu na umoja wa Kiislamu na bila shaka upuuzaji wowote kuhusu suala hilo muhimu na nyeti la ulimwengu wa Kiislamu ni hiana ya wazi kwa malengo matukufu ya Wapalestina. Ushirikiano hatari na muovu wa Marekani, Israel na Saudi Arabia umekuwa na madhara makubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo kama vile ambavyo muhimili wa mapambano kwa kuwa na mwamko wa kutosha kuhusiana na pembe tatu hiyo ya shari, umefanikiwa kuwatokomeza matakfiri wa Daesh nchini Syria na Iraq, mara hii pia, kwa kudumisha umoja wa Kiislamu na kutokana na radiamali erevu ya Wapalestina, utafanikiwa kuvunja njama hii mpya inayotekelezwa dhidi ya Quds Tukufu. Uzoefu unaonyesha wazi kwamba Intifadha tofauti za Wapalestina zimeweza kuvunja njama mbalimbali zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Quds Tukufu na bila shaka kudumishwa mwenendo huo kutavunja njama mpya za maadui dhidi ya Kibla hicho cha kwanza cha Waislamu. Hasira ya Wapalestina iliyodhihirishwa kupitia uchaomaji moto wa picha za Rais Donald Trump wa Marekani, ni utangulizi wa radiamali yao kuhusu utendaji wa serikali yake kuhusiana na suala la Quds. Jambo hilo linathibitisha wazi kuwa iwapo Trump atatekeleza ahadi yake ya kuhamishia Quds ubalozi wa Marekani basi kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, suala hilo litatoa pigo kubwa na la kuwaangamiza Wazayuni.
Ushindi wa muhimili wa mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh unatilia mkazo umuhimu wa kuwepo Umoja wa Kiislamu kuliko wakati mwingine wowote ule. Umoja wa Kiislamu na Mapambano dhidi ya njama za maadui ni njia ya uhakika ya kufikia nguvu na utukufu wa ulimwengu wa Kiislamu. Kwa kutilia maanani uwezo mkubwa wa jamii na nchi za Kiislamu, nji hii ni laini kabisa na hivyo ili kufikia nguvu hiyo panahitajika kuwepo mshikamano wa Kiislamu katika kukabiliana na njama zisizokoma za maadui kuhusu masuala mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu, na hasa suala la Quds Tukufu na Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.