Mkutano wa Umoja wa Kiislamu waunga mkono Intifadha mpya ya Palestina
Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umemalizika mjini Tehran kwa kutoa taarifa yenye vipengee 26 inayosisitiza kuimarishwa umoja wa Kiislamu kwa ajili ya kupambana na njama za maadui, ikiwemo njama mpya ya Marekani dhidi ya Quds Tukufu.
Mkutano huo ulioanza siku ya Jumanne mjini Tehran ulimalizika Alkhamisi usiku. Tarifa ya mwisho ya mkutano huo imezingatia masuala mawili muhimu. La kwanza ni kuwa, kwa kutilia maanani uwezo mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu, kuhuishwa ustaarabu wa Kiislamu kwa lengo la kuokoa jamii ya mwanadamu kutokana na machungu anayoyapitia ni jambo la dharura. Suala la pili ni kulaaniwa hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani ya kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran wamesisitiza udharura wa kukabiliana na siasa mpya za Marekani za kuuyahudisha mji mtakatifu wa Quds na kudhibiti matukufu ya Waislamu na kusisitiza kuwa Ulimwengu wa Kiislamu inahitajia Intifadha ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na njama mpya ya maadui dhidi ya Beitul Maqdis.

Kikao cha mwisho cha Mkutano wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran
Baada ya kuangamizwa magaidi wa kitakfiri wa Daesh nchini Syria na Iraq, maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu wameanzisha njama mpya dhidi ya matukufu ya Kiislamu. Lengo la njama hiyo ni kuudhaminia amani na usalama utawala ghasibu wa Israel kupitia ushirikiano wa baadhi ya watawala vibaraka na wasaliti wa Kiarabu. Jumatano usiku, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na wakati huohuo kutoa amri ya kuhamishiwa katika mji huo ubalozi wa Marekani kutoka mjini Tel Aviv. Hata kama uamuzi huo wa Trump hautabadili ukweli wa kihistoria na kiutambulisho wa mji wa Quds, lakini lililo wazi ni kuwa njama hiyo mpya inatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu wa baadhi ya nchi saliti za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel. Tunachotaka kusema ni kuwa hatua ya nchi hizo za Kiarabu ya kurejesha uhusiano wao wa kawaida na utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, imechangia pakubwa kumshajiisha Trump achukue uamuzi wa kutangaza Quds Tukufu kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni. Kuhusu suala hilo, Faisal Miqdad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema: Ushirikiano wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi katika mkondo wa njama dhidi ya Palestina, ni sababu kuu iliyoichochea serikali ya Trump kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Quds.

Hatua mpya ya Trump dhidi ya mji huo mtakatifu inatoa udharura wa Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na mwamko na kutahadhari zaidi. Umoja wa Umma na serikali za Kiislamu ni suala muhimu ambalo iwapo litazingatiwa na kupewa umuhimu unaofaa, halitatoa mwanya wowote wa kutekelezwa njama dhidi ya nchi za Kiislamu. Uungaji mkono wa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kwa Intifadha mpya ya Palestina katika mazingira ya sasa ya kutekelezwa njama dhidi ya mji mtakatifu wa Quds, ni ishara ya wazi ya kuwepo umoja kuhusiana na malengo matukufu ya Palestina na umuhimu wa kuwa macho mbele ya njama mpya zinazofanywa na maadui dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kumalizika fitina ya Daesh katika nchi za Syria na Iraq sasa umewadia wakati wa kulipa umuhimu wa kwanza suala la Quds na Palestina.

Kwa kufuatilia kwa karibu matukio ya Palestina na kunufaika na uwezo wao tofauti, nchi za Kiislamu bila shaka zitavunja njama hii mpya dhidi ya Quds Tukufu. Hakuna nchi wala rais yeyote anayeweza kuainisha mustakbali wa Quds bali ni historia na irada ya waungaji mkono wa malengo matukufu ya Palestina ndiyo itakayoainisha mustakbali huo. Uungaji mkono kwa Intifadha mpya ya Palestina kwa lengo la kuulinda mji wa kihistoria na mtakatifu wa Quds ni matarajio muhimu ya watetezi wa malengo hayo matukufu. Katika uwanja huo, Tayari Wapalestina wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kuanzisha Intifadha mpya ya kuikomboa Quds. Uzoefu unathibitisha wazi kwamba mapambano ndiyo njia pekee ya kuikomboa Palestina na kuzima njama za maadui. Kuhusiana na hilo Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Kisiasa ya Harakati ya Kiislamu ya Palestina HAMAS anasisitiza kwa kusema: Njia pekee ya kukabiliana na siasa za Israel zinazoungwa mkono na Marekani ni Intifadha mpya na Wapalestina watatekeleza majukumu yao kupitia Intifadha hiyo mpya.