Rais Rouhani: Maadui wamekasirishwa na maendeleo ya Iran
(last modified Mon, 01 Jan 2018 16:13:35 GMT )
Jan 01, 2018 16:13 UTC
  • Rais Rouhani: Maadui wamekasirishwa na maendeleo ya Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mafanikio ya taifa la Iran katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kikanda yamewatia hasira na kuwaghadhibisha maadui.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika kikao cha viongozi wa kamati za kitaalamu za Bunge la Iran. Ameashiria malalamiko na mikusanyiko ya siku kadhaa zilizopita katika baadhi ya maeneo ya Iran na kusema: Ukosoaji na malalamiko ya wananchi ni fursa na si tishio, na taifa la Iran litatojibu kwa wale wanaovunja sheria na kusababisha machafuko.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya wananchi katika miji kadhaa ya Iran walifanya maandamano wakilalamikia kutokuchukuliwa hatua za kushughulikia watu waliopoteza fedha zao katika taasisi za fedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na usimamizi dhaifu wa serikali katika baadhi ya sekta. Baadhi ya maandamano hayo yametumiwa vibaya na wahalifu na kusababisha machafuko.

Rais Rouhani amesema kuwa, ushindi wa kisiasa wa taifa la Iran duniani ikiwa ni pamoja kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, mafanikio yake katika kupambana na ugaidi eneo la Mashariki ya Kati na kushindwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni miongoni mwa sababu kuu za uadui wa serikali ya Washington na baadhi ya nchi za kanda hii dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa kwa sasa Iran ina mchango mkubwa katika kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuangamiza ugaidi, katika mustakbali wa Syria, kurejesha utulivu kamili katika nchi za Iraq na Libanon na katika kutetea watu wanaodhulumiwa kote duniani. 

Amesema mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwiba katika jicho la maadui na hayastahamiliki kwa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Ameongeza kuwa maadui hao wamekuwa wakiwania fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya taifa la Iran.

Rais Rouhani amesema, kuwepo baadhi ya matatizo kiuchumi hapa nchini ni jambo ambalo haliwezi kukanushwa lakini amesisitiza kuwa, taifa la Iran litavuka matatizo hayo na kutoa jibu kwa wale wanaosababisha ghasia na machafuko, wanaovunjia heshima matukufu na thamani za kimapinduzi na kuharibu mali za umma.        

Tags