Shamkhani: Iran kamwe haitaacha kuwaunga mkono wananchi wa Palestina
(last modified Wed, 03 Jan 2018 07:39:38 GMT )
Jan 03, 2018 07:39 UTC
  • Shamkhani: Iran kamwe haitaacha kuwaunga mkono wananchi wa Palestina

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa lengo la kutaka kujadiliwa na kufanyika mazungumzo kuhusu Palestina ni kuisahaulisha kadhia ya Palestina na kwamba kuharibiwa ardhi hiyo ni lengo kuu la maghasibu ambao wanafanya njama za kuzikalia kwa mabavu ardhi zote za Palestina.

Akizungumza na kanali ya televisheni ya al Mayadin ya Lebanon, Ali Shmkhani ameashiria hatua ya Rais wa Marekani ya kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa Marekani unamaanisha kumalizika mazungumzo kuhusu Palestina; na kwamba hatua hiyo ya Donald Trump imepelekea kuwepo umoja  ndani ya Palestina. 

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameeleza kuwa kumejitokeza imani hii katika fikra za vijana wa Kipalestina na wasio Wpalestina kwamba muqawama ndio njia pekee ya kukabiliana na maghasibu. Ali Shamkhani ameongeza kuwa kupanuka fikra za muqawama na kufichuliwa sura ya uistikbari ni moja ya uungaji mkono wa Iran kwa kadhia ya Palestina na kwamba Iran haitasitisha uungaji mkono wake kwa wananchi wa Palestina, kadhia ya Palestina na mapambano yao ya ukombozi.

Vijana wa Kipalestina katika mapambano ya Intifadha dhidi ya maghasibu wa Kizayuni

Kuhusu tuhuma za Marekani kwamba Iran inatoa msaada wa makombora kwa Yemen, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameeleza kuwa tuhuma hizo zimetolewa ili kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusu kushiriki Marekani katika jinai za Saudi Arabia huko Yemen. Hii ni kwa sababu wananchi wa Yemen wenyewe wanazo silaha za kistratejia na hawahitajii msaada wa Iran.