Iran: Ushirikiano wa dunia unahitajika kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani milipuko ya kigaidi iliyotokea huko Benghazi Libya ambapo mbali na kuwapa mkono wa pole wale waliopoteza ndugu zao katika tukio hilo la kigaidi amesenma kuwa, ili kuukabiliana na ugaidi usio na mipaka kuna haja ya kuweko ushirikiano wa dunia katika hilo.
Bahram Qassemi amebainisha kwamba, baada ya ugaidi usio na mipaka kusambaratishwa kwa fedheha katika eneo la Mashariki ya Kati umeendelea kufanya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kwamba, ili kukabiliana na vitendo vya ugaidi usio na mipaka kuna haja ya kuweko ushirikiano wa kilimwengu.
Watu wasiopungua 33 wameuawa na wengine wapatao 50 wamejeruhiwa baada ya magari mawili yaliyotegwa mabomu kuripuka katika mji wa Benghazi ulioko mashariki mwa Libya.
Ahmad Al- Faituri, kamanda wa kitengo cha upelelezi na utiaji nguvuni katika jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulio hayo.
Miripuko hiyo ya mabomu imevuruga utulivu wa kiwango fulani uliokuwa umerejea hivi karibuni kwenye mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Libya.
Amani na uthabiti vimetoweka nchini Libya tangu mwaka 2011 kutokana na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo kufuatia mapinduzi ya wananchi yaliyohitimisha utawala wa miongo kadhaa wa Muammar Gaddafi.
Mataifa mbalimbali yamelaani mashambulio hayo ya kigaidi nchini Libya ambayo kimsingi yanakwamisha juhudi za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.