Zarif arudisha mapigo, asema Saudia na Marekani waliisaidia Daesh kwa silaha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif amesema Saudi Arabia na Marekani haziwezi kupotosha ukweli wa mambo kuhusu misaada na ufadhili wao kwa kundi la kigaidi la Daesh.
Zarif ambaye alikuwa akijibu madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika Jukwaa la Kiuchumi la Davos huko Uswisi, amesema makelele ya kipropaganda ya Donald Trump Rais wa Marekani na Saudi Arabia yanayodai kuwa pande hizo mbili zimelishinda kundi la kigaidi la Daesh hayawezi kubadilisha uhakika na ukweli wa mambo.
Amesema Marekani na Saudi Arabia zililisaidia kundi hilo kwa silaha huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiharakia kuwasadia watu wa Iraq na Syria kwa ajili ya kuliangamiza kundi hilo la kitakfiri na kigaidi la Daesh.
Akihutubia kikao cha Davos, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al Jubair amedai kuwa Iran inachochea migawanyiko ya kimadhehebu katika eneo la Mashariki ya Kati.
"Marekani na Saudi Arabia haziwezi kubadili uhakika kuhusu mchango mkubwa wa Iran katika kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh", amesisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu.
Saudi Arabia inatambuliwa kuwa ngome na chimbuko na mawahabi na matakfiri wanaofanya ukatili na mauaji ya kutisha kwa kutumia jina safi la Uislamu. Nchi hiyo pia ni mfadhili mkubwa wa kifedha na silaha kwa makundi ya kigaidi kama lile la Daesh ambalo lilianzishwa kwa fedha za mafuta za nchi hiyo.