Mufti wa Waislamu wa Kisuni Iraq ayasifu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
(last modified Sat, 10 Feb 2018 07:57:22 GMT )
Feb 10, 2018 07:57 UTC
  • Mufti wa Waislamu wa Kisuni Iraq ayasifu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Mufti Mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Kisuni nchini Iraq ameyasifu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kueleza kuwa, yamekuwa na taathira chanya katika Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla.

Sheikh Abdul Mahdi al-Sumaidaie amesema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 39 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kubainisha kwamba, mapinduzi hayo yaliyopata ushindi kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA yamekuwa na nafasi kubwa na muhimu katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Mufti Mkuu wa Waislamu wa Kisuni nchini Iraq amesema kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamepitia changamoto nyingi vikiwemo vita, lakini hivi sasa Alhamdulilahi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali ndani na nje, na yote hayo ni matunda ya Mapinduzi haya ya Kiislamu yaliyotokea mwaka 1979.

Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 

Mufti Abdul Mahdi al-Sumaidaie ameongeza kuwa, hii leo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuwa na athari chanya na kwamba athari hizo nzuri zinaonekana huko Sudan, Somalia, Yemen, Iraq, Afghanistan na hata katika baadhi ya madola ya Magharibi.

Amesema, Iran imepiga hatua kubwa ya ustawi licha ya njama za madola ya kibeberu  na vikwazo vyao dhidi ya taifa hili.

Kadhalika Mufti wa Waislamu wa Kisuni nchini Iraq amesema kuwa, Iran imekuwa na nafasi muhimu mno katika kuitetea na kuiunga mkono kadhia ya Palestina pamoja na harakati za kupigania ukombozi duniani bila kusahau uungaji mkono wake kwa wanamuqawama huko Lebanon, Palestina , Iraq na Syria.

Tags