Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani anaeneza chuki dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Mshauri wa Usalama wa Taifa katika utawala wa Marekani anaeneza chuki dhidi ya Iran.
Wakati akihutubu katika Kikao cha 54 cha Usalama cha Munich nchini Ujerumani siku ya Jumamosi, Herbert Raymond McMaster Mshauri wa Usalama wa Taifa katika serikali ya Marekani alitoa wito kwa waitifaki wa Marekani kusitisha biashara na Iran kwa madai kuwa nchi hii inaingilia mambo ya ndani ya eneo. Kwa mara kadhaa sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha tuhuma hizo na kuzitaja kuwa zisizo na msingi.
Kufuatia matamshi ya McMaster, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi ametoa taarifa na kusema matamshi hayo ni sehemu ya sera zinazofeli za Marekani za kueneza chuki dhidi ya Iran au Iranophobia.
Amesema matamshi ya afisa huyo wa ngazi za juu nchini Marekani yanalenga kuizuia Iran kunufaika na mapatano ya nyuklia baina yake na madola sita makubwa duniani. Mapatano hayo ya nyuklia ambayo rasmi yanajulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, yalifikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na nchi za 5+1 ambazo ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani.
Qassemi amesema hatua ya nchi nyingi kuwania kuwekeza nchini Iran baada ya mapatano ya JCPOA ni jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa wakuu wa Marekani.
Aidha amesema kufeli sera za Marekani kote duniani ni jambo ambalo limeifanya serikali ya Washington kupoteza itibari na kukosa kutegemewa.