Zarif azikosoa nchi za Ulaya kwa kukubali mashinikizo ya Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa baadhi ya matamshi na mienendo ya viongozi wa nchi za Ulaya kuhusuna na utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na vilevile tabia yao ya kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mazungumzo yake na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian aliyeko safari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, makubaliano ya pande kadhaa ya nyuklia ya JCPOA ambayo kwa mujibu ripoti 10 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Iran imeyatekeleza kikamilifu, sasa yanakabiliwa na michezo ya kisiasa ya isiyo ya kimantiki ya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Ulaya inapaswa kutekeleza kikamilifu majukumu yake kuhusu makubaliano hayo na kuishinikiza Marekani ili nayo iheshimu na kutekeleza majukumu yake. Amesisitiza kwamba nchi za Ulaya hazipasi kuiruhusu Marekani kutoa matakwa yasiyo ya kimantiki licha ya kuendelea kukiuka makubaliano ya JCPOA.
Zarif pia ameashiria mapendekezo yaliyotolewa na Iran kwa ajili ya kutatua migogoro ya kikanda na kusema: "Kama kweli Ulaya inataka kukomesha maafa ya kibinadamu katika eneo la Mashariki ya Kati inaweza kufaidika na mabadilishano ya maoni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja huo; na kama lengo ni kufanya propaganda na kutaka kuiridhisha Marekani, basi ijue kwamba Iran haitaingia katika mchezo huo."
Waziri wa Mambo ya Nje amesema kuwa, suala la uwezo wa makombora ya Iran liko nje kabisa ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hata azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesisitiza kuwa, Marekani na nchi nyingine ambazo zimelifanya eneo la Mashariki ya Kati kama ghala kubwa la baruti kutokana na kuziuzia silaha kwa wingi nchi za eneo hili zinapaswa kusitisha hatua hizo. Muhammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, uwezo wa makombora ya Iran ni kwa ajili ya kulinda nchi na raia wake.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian ameashiria hatua zilizochukuliwa na nchi yake kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika miradi ya viwanda vya magari na sekta ya nishati hapa nchini.
Jean-Yves Le Drian amesema Ufaransa itaendelea kufanya jitihada za kuimarisha uhusiano wake wa kirafiki na Iran na kuongeza kuwa, Ulaya hususan Ufaransa itaendelea kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA licha ya mashinikizo ya Marekani.