Zarif aanza safari ya kuzitembelea nchi za Afrika, Amerika ya Latini
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran leo Jumapili ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Kiafrika na Amerika ya Latini.
Mohammad Javad Zarif anaongoza ujumbe mkubwa wa viongozi wa serikali na wawekezaji katika safari hiyo rasmi ya kikazi.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Dakta Zarif na ujumbe wake watazitembelea nchi za Senegal, Namibia, Brazil na Uruguay.
Mbali na wawakilishi wa mashirika ya Iran, Zarif anaandamana pia na wajasiriamali kutoka sekta za biashara, uchumi na sayansi wa hapa nchini.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa nchi nne hizo katika nyuga za siasa, uchumi, na bunge.
Kadhalika anatazamiwa kuhutubia mikutano ya uchumi na biashara katika nchi hizo, mbali na kukutana na wanafikra mbalimbali.
Itakumbukwa kuwa, mwezi Oktoba mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran alizitembelea nchi nyingine za Afrika za Uganda, Afrika Kusini na Niger.